Timu ya kamba wanaume Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakivuta kamba dhidi ya Hazina (hawapo pichani) ambapo timu hizo zimetoshana nguvu kwa kuvutana 1-1 katika Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya kamba wanaume kutoka Wizara ya Ujenzi wametoshana nguvu kwa mvuto 1-1 na watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) katika Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya Mahakama (kulia) wakivuta kamba dhidi ya Polisi (kushoto) katika Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Morogoro.
Mchezaji wa timu ya Netiboli kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Jackline Matiko (WA) akiwadhibiti kwa kufuata mpira wachezaji wa timu ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (waliovaa jezi ya njano) ambapo timu hiyo iliibuka washindi kwa jumla ya magoli 34-09 katika Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Morogoro.
……………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi,Morogoro
Mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanaendelea kushika kasi mjini Morogoro huku watumishi wakipata muda mujarabu wa kufanya mazoezi hatua inayowasidia kuimarisha afya zao.
Ni siku ya saba tangu mashindano hayo yaanze Oktoba 20, 2021 na yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango katika kiwanja cha Jamhuri mkoani Morogoro.
Leo Oktoba 26, 2021 imechezwa michezo mitatu ambayo ni kamba wanaume na wanawake, netiboli pamoja na mpira wa miguu hatua ya makundi.
Kwenye mchezo wa kamba wanaume timu ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wametoka suluhu kwa kututana na Hazina (1-1), Wizara ya Ujenzi wametoshana nguvu na wenzao wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (1-1) na Ukaguzi nao wametoshana nguvu na Wizara ya Madini.
Timu nyingine zilizocheza leo zimewavuta timu pinzani kwa mivuto miwili (2-0) ni Wizara ya Kilimo dhidi ya Ulinzi, Wizara ya Uchukuzi dhidi ya Wizara Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii dhidi ya Wizara ya Katiba na Sheria, timu ya Mahakama dhidi ya Polisi, Tume ya Uchaguzi (NEC) dhidi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Maji dhidi ya Ulinzi, Wizara ya Ujenzi dhidi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kwa upande wa Kamba wanawake timu zote zilizocheza leo zimeshinda kwa kuwavuta wapinzani wao mara zote mbili (2-0) ambapo Wizara ya Madini wameivuta timu ya Wizara ya Ujenzi, timu ya Wizara ya Kilimo dhidi ya Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Ofisi ya Waziri Mkuu dhidi ya Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii dhidi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katika mchezo wa netiboli, timu ya Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro imewafunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa jumla ya magoli 34-09, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wameifunga timu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa jumla ya magoli (30-09) na timu ya Hazina wameifunga timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jumla ya magoli (31-06).
Kwa upande wa mchezo wa mpira wa miguu, timu ya Wizara ya Ujenzi imewafunga timu ya wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (OSHA) kwa 1-0, timu ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wametoshana nguvu bila kufungana na timu ya Wizara ya Maji, Wizara ya Madini wametoshana nguvu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kufungana goli 1-1, Wizara ya Katiba na Sheria wameifunga timu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa jumla ya magoli 4-0 huku Hazina wakipata ushindi dhidi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Mashindano hayo kwa siku ya kesho yanatarajiwa kuendelea kwa mchezo wa riadha kwa wanaume na wanawake utakaoanza kuchezwa kuanzia saa 1:00 asubuhi kwa mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500 pamoja na mita 100 kukimbizana vijiti.