Home Michezo WANARIADHA VIJANA NA WAZEE KUSHINDANA SHIMIWI KESHO

WANARIADHA VIJANA NA WAZEE KUSHINDANA SHIMIWI KESHO

0

…………………………………………………

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WANARIADHA vijana na wazee kutoka Wizara, Idara na Sekretarieti za mikoa kesho watashindana kwenye mbio za riadha za mita 100, 200, 400, 800, 1,500 na kupokezana vijiti (relay x100) kwenye michuano ya michezo ya Shirikisho la michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) itakayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mbio hizo zimegawanywa kwa umri  ambapo kwa upande wa wachezaji wazee kuanzia miaka 55 hadi 59 watachuana wenyewe kwa wenyewe kwenye mita 100 pekee kwa wanaume na wanawake, wakati wanariadha wengine wenye umri wa kuanzia miaka 25  watacheza mita mbalimbali ikiwemo kurusha tufe.

Hatahivyo katika michezo iliyofanyika leo ya kuvuta kamba kwa upande wa wanawake timu ya Wizara ya Madini waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) kwa 2-0; huku Wizara ya Kilimo wakiwaadabisha RAS Ruvuma kwa 2-0; nao Ofisi ya Waziri Mkuu waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa 2-0; na Wizara ya Maliasili na Utalii waliwachakaza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mivuto 2-0. 

Kwa upande wa wanaume timu ya Uchukuzi wanaume waliwavuta Wizara ya Maji kwa mivuto 2-0; huku Wizara ya Maliasili na Utalii waliwavuta Wizara ya Katiba na Sheria kwa 2-0; nao Idara ya Mahakama waliwavuta Polisi kwa 2-0; wakati Tume ya Uchaguzi (NEC) waliwaadabisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa 2-0; huku Wizara ya Maji waliwavuta Ulinzi kwa 2-0 na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Ujenzi) waliwavuta Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa 2-0.

Katika michezo mingine ya kuvuta kamba wanaume timu ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari walitoshana nguvu na Hazina kwa 1-1; huku Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Ujenzi) walitoana jasho na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa 1-1; nao Wizara ya Madini na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali walitoka sare ya 1—1.

Katika michezo ya netiboli timu ya Wizara ya Elimu iliwafunga Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa magoli 30-9, washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 20-4; nao Hazina waliwafunga Wizara ya Maliasili na Utalii kwa magoli 31-6 washindi waliongoza kwa magoli 19-4; wakati RAS Moro waliwafunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa magoli 34-9, ambapo hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 14-4.

Katika mchezo wa soka uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Jordan timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) waliwafunga Wakala wa Usalama na Afya mahala pa Kazi (OSHA) kwa goli 1-0; katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Moro timu ya Wizara ya Maji walitoka suluhu na Tamisemi.

Wakati Wizara ya Katiba na Sheria wamewafunga Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa magoli 4-0 na Wizara ya Madini na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walitoka sare ya  bao 1-1 michezo hiyo ilifanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA – Kampasi ya Mazimbu); nao Hazina wamewashinda Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika mchezo uliofanyika uwanja wa Jamhuri.

Michuano hiyo inatarajia kufika kilele tarehe 2 Novemba, ambapo washindi watazawadiwa zawadi mbalimbali vikiwemo vikombe.

MWISHO

.