………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKOA wa Pwani umepokea chanjo nyingine ya Uviko 19 ,awamu ya pili ,aina ya Sinopharm inayotengenezwa nchini China zipatazo 25,000 ili kujikinga na ugonjwa huo.
Aidha mkoa huo hauna mgonjwa wa Uviko 19 kwasasa hivyo wananchi wameaswa kujitokeza kuendelea kujikinga na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kupambana na ugonjwa huo.
Akizungumza chanjo hiyo ,katika kikao Cha viongozi wa mkoa kuhusiana na utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19 ,kilichofanyika ukumbi mkubwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ,mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Dkt.Gunini Kamba alisema dozi hii nayo ni salama ,haina madhara hata kwa wajawazito kama ilivyo kwa dozi ya JJ.
“Dozi ya chanjo hii ya Sinopharm itatakiwa kuchomwa mara mbili ambapo ukichanja lazima urudie dozi ya pili baada ya siku 28, na hata ukichelewa kurudi baada ya muda huo kwa wiki haitokuwa na madhara kwani ni lazima uchanje Tena”alifafanua Gunini.
“Katika hii dozi pia mtu mmoja atachanja kichupa kimoja , tofauti na dozi ya JJ ambayo kichupa kimoja kilitakiwa kuchomwa watu watano ,”alisisitiza .
Gunini alibainisha kati ya chanjo hizo halmashauri ya Bagamoyo imepata dozi 4,000, Chalinze 3,000,Kibaha Vijijini 2,000,Kibiti 2,000,Kibaha Mjini 4,000 , Kisarawe 3,000,Mafia 1,000,Rufiji 3,000 na Mkuranga 3,000.
Hata hivyo alielezea ,awali agost mwaka huu walipokea dozi 30,000 mwitikio haukuwa mzuri kwakuwa watu walikuwa hawana elimu .
Gunini alisema kwamba ,baadae zoezi lilifanikiwa kutokana na watu kuanza kuwa na uelewa juu ya umuhimu wa chanjo na wakaomba nyongeza ya dozi 1,200 ambazo zote zimekwisha .
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani , Abubakari Kunenge alisema Kwa juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan amewezesha kupata mkopo wenye masharti nafuu sh.trilioni 1.3 kutoka shirika la fedha la kimataifa (IMF) kwa ajili ya Mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19.
Alisema hatua za utekelezaji wa mpango huo zimeanza , wataalamu wameshakutana na kuandaa mikakati na mipango kazi chini ya usimamizi wa katibu Tawala mkoa wa Pwani.
Kunenge alihimiza, halmashauri kuwa na Mpango kazi wenye kuhakikisha utekelezaji unafanikiwa kwa muda uliopangwa.
“Niwatake wananchi waendelee kupambana na ugonjwa wa Uviko 19, tuondokane na vishawishi kuwa chanjo zina madhara ,wajitokeze kuchanja na tusimwangushe kwa hili Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan,
Katibu Tawala mkoa , Mhandisi Mwanasha Tumbo alielezea mkoa wa Pwani umeidhinishiwa sh.bilioni 13.390 kwa utekelezaji wa miradi ya elimu na afya ambapo vyumba vya madarasa 422 ya shule ya sekondari,vyumba vya madarasa 108 ya vituo shikizi 37 vya shule za msingi, ujenzi wa mabweni manne na nyumba Saba za watumishi wa afya, ununuzi wa mashine mbili za mionzi ,ICU na ujenzi wa majengo matatu ya huduma za dharura.