Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society(FCS), Francis Kiwanga,akiongoza majadiliano ya utekelezaji wa Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa miaka mitano katika Wiki ya Azaki inayoendelea katika hoteli ya Royal jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga,akizungumza wakati wa majadiliano ya utekelezaji wa Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa miaka mitano katika Wiki ya Azaki inayoendelea katika hoteli ya Royal jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia mada mbalimbali wakati wa majadiliano ya utekelezaji wa Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa miaka mitano katika Wiki ya Azaki inayoendelea katika hoteli ya Royal jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………….
Na Alex Sonna, Dodoma
Asasi za Kiraia(AZAKI) zimeanza leo majadiliano ya namna zitakavyochangia kwenye utekelezaji wa Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa miaka mitano.
Akizungumza kwenye majadiliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society(FCS), Francis Kiwanga, amesema katika Wiki ya Azaki kutakuwa na mijadala mikubwa na huru ambayo imegawanywa kwenye sehemu mbalimbali yaliyofanyika leo Oktoba 25,2021 katika hoteli ya Royal jijini Dodoma.
“Siku hii ya kwanza itakuwa ni kuangalia sisi kama asasi za kiraia mchango wetu kwa maendeleo ya taifa letu, kama mnakumbuka wiki tatu zilizopita Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na sekta na kuzindua taarifa iliyoandaliwa na Wizara kuhusu mchango wa asasi katika maendeleo ya taifa, tuliona mchango mkubwa sana katika masuala ya elimu, ajira, kodi na kuleta fedha ambapo tuliona zaidi ya Sh.Bilioni 1.4 zinaingia kwenye uchumi wa taifa letu kupitia Azaki,”amesema.
Amesema watajadili kwa kina katika kupambana na adui wa umaskini, ujinga na maradhi kwa kuwa wana wajibu wa kusaidia maendeleo kujenga ustawi kwa jamii.
“Nafurahi tumezindua Mpango wa Maendeleo ya Miaka mitano lakini ni kwa kiasi gani kwa mfano sekta zote za serikali zinatambua mpango na kuchangia kwenye kutekeleza, sekta binafsi wanashiriki vipi kwenye mpango, sisi Azaki tunachangia vipi,”amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema asasi zimekuwa na mchango mkubwa katika utawala wa sheria huku akisema endapo zitakuwa haziwajibiki vyema watakaoathirika ni wananchi.
“Asasi zinafanya kazi kubwa ya kuziangalia sheria kabla hazijaenda bungeni kwa mfano sisi asasi ambazo zinajihusisha na sheria moja kwa moja hakuna muswada unaokwenda bungeni bila kuhusishwa sisi wadau, tunashukuru kwa huo ushirikano, hata sheria ya NGOs ilivyokuwa inakuja ilikuwa na changamoto nyingi kuliko hizi sasa hivi LHRC tulichambua na asilimia 33 ya mapendekezo yetu yalichukuliwa,”amesema.