Na Joseph Lyimo
“Miongoni mwa malengo yetu ni kuelimisha jamii ya kifugaji ili kuwasomesha, kuwafuatilia na kuwasaidia watoto wa jinsia zote ili waweze kufikia ndoto zao wa ustawi wa elimu,” Hivi ndivyo anavyoanza kwa kusema Katibu Mkuu wa shirika la Elimisha Simanjiro Organization (ESO) Lowassa Edward Lekor, wakati akizungumza juu ya uzinduzi wa kampeni ya niache nisome yenye lengo la kusaidia jamii ya eneo hilo ili watoto wa kifugaji wapate elimu.
Lowassa anasema vijana wasomi wa Wilaya ya Simanjiro, kupitia shirika la Elimisha Simanjiro Organization (ESO) wameanzisha kampeni ya niache nisome yenye lengo la kusaidia watoto wa jamii ya kifugaji kusoma.
Amesema shirika la Elimisha Simanjiro limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwafikia wananchi waishio Simanjiro na kutoa elimu na hamasa juu ya umuhimu wa kuwasomesha watoto hasa mtoto wa kike.
“Ziara zote tulizozifanya mashuleni zimeleta mabadiliko makubwa kifikra kwa wanafunzi kwani wameonyesha kuwa wakiwezeshwa wanaweza na adui yetu ni ujinga na silaha yetu ni umoja,” amesema Lowassa.
Amezitaja kata tisa kati ya 18 walizofika kwenye shule za msingi na sekondari ni Langai, Terrat, Orkesumet, Msitu wa Tembo, Kitwai, Oljoro Namba 5, Loiborsoit, Naberera na Edonyongijape.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Batenga, amewapongeza ESO kwa kuanzisha kampeni hiyo ya niache nisome kwani itawanyanyua watoto wa kifugaji.
Batenga amesema mwamko wa elimu kwa jamii ya kifugaji ni mdogo hivyo kupitia kampeni hiyo watoto wengi wa kifugaji watafaidika na elimu.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, amewataka vijana hao kuhakikisha wanapambana na maendeleo na kutohusisha shirika lao na masuala ya kisiasa.
Ole Sendeka amesema lengo lao ni zuri kwani litachochea watoto wengi wa eneo hilo kupata elimu na kufanikisha maendeleo ya eneo hilo.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, bilionea Saniniu Laizer ambaye amechangia shilingi milioni 5 kwa shirika hilo aliwapongeza ESO kwa kuanzisha kampeni hiyo.
Bilionea Laizer amesema elimu ndiyo ukombozi kwa jamii ya kifugaji hivyo wanapaswa kushirikiana katika kutekeleza hilo ili wasichana wasome wasiozeshwe na wavulana wasome wasichunge mifugo.
Diwani mstaafu wa Kata ya Oljoro Namba tano, Mathayo Lormuje amesema amesema yeye ni miongoni mwa wazazi wa jamii ya wafugaji waliosomesha watoto bila kubagua jinsia.
“Mimi nimesomesha watoto saba bila kubagua wakike au wa kiume na wengine watatu watajiunga na shule hivi karibuni hivyo wafugaji tusomeshe watoto wetu,” amesema Lormuje.
Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amesema kupitia mifugo walionayo, jamii ya wafugaji wanapaswa waitumie kama utajiri ili wawape elimu watoto wao.