Home Biashara TRA YATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA KUJIEPUSHA NA BIASHARA ZA MAGENDO

TRA YATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA KUJIEPUSHA NA BIASHARA ZA MAGENDO

0

Afisa Forodha Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Muhidini Mwalugoya (aliyesimama) akitoa elimu kuhusu athari za magendo kwa wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu atahri za magendo katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.

Baadhi ya Wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje wakifuatilia elimu kuhusu athari za magendo iliyokuwa ikitolewa na Afisa wa TRA (hayupo pichani) hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu atahri za magendo katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.

Afisa Forodha Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ernest Mngube (aliyesimama) akitoa elimu na kujibu maswali kuhusu athari za magendo kwa wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu atahri za magendo katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.

Mwandishi Wetu.

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA (TRA), imewataka wafanyabiashara nchini kujiepusha na biashara za magendo wakati wanapofanya shughuli zao za kibiashara katika maeneo yao ili wao wenyewe pamoja jamii inayowazunguka wasiathirike na athari zitokanazo na biashara hiyo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Afisa Forodha Mwandamizi wa TRA, Bw. Muhidini Mwalugoya wakati wa kampeni maalum ya utoaji elimu kuhusu athari za magendo katika mikoa ya ya Lindi na Mtwara.

Bwana Mwalugoya amesema kwamba kufanya biashara za magendo kunaweza kuleta athari nyingi katika jamii kiafya, kiuchumi na kiusalama wa nchi akafafanua kuwa, inapotokea wafanyabiashara wanaingiza bidhaa zao kupitia njia zisizo rasmi maarufu kama njia za panya, jamii ya eneo husika huathirika, kwa mfano uingizaji wa vyakula au bidhaa zisizo na viwango ama zilizopita muda wake wa matumizi kunaweza pelekea mlipuko wa magonjwa na kuathiri wananchi.

Aliongeza kuwa, athari nyingine zitokanazo na biashara ya magendo ni pamoja kiusalama wa nchi, baadhi ya watu wasio na lengo zuri ama waharifu wanaweza kuingiza nchini bidhaa ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi, mfano kuingiza silaha au risasi ambazo baadaye zinaweza kusambaa katika jamii na kuleta machafuko.

“Watanzania wenzangu, athari za kufanya biashara za magendo ni nyingi hivyo lazima tuhakikishe kuwa tunaelimishana ili wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla waachane na kufanya biashara za namna hii, kwa mfano tukiendekeza kupitisha bidhaa kutoka nje ya kwa njia zisizo rasmi tunaweza kuathiri uchumi wa nchi yetu pia, kwasababu zitakua hazilipi kodi na matokeo yake tunakosa mapato stahiki ya kutuletea maendeleo nchini, hivyo niwaombe sasa tuachane na hizi biashara”, alisema Mwalugoya.

Aidha, amewataka wafanyabiashara na wananchi nchini kuhakikisha kuwa wanatumia njia zilizo rasmi katika kupitisha bidhaa zao ili TRA iweze kukusanya mapato na pindi wapatapo changamoto yoyote wasisite kuwasiliana naMaofisa wa TRA katika maeneo husika ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya Ulinzi na usalama mara waonapo baadhi ya watu au kikundi cha watu wanafanya biashara za magendo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.