Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria akitoa maelekezo yakutaka kuwachukulia hatua za kisheria wazazi watakaopatikana na hatia ya kutengeneza kesi za ubakaji ili kujipatia fedha. ametoa maelekezo yake hivi karibuni Mkoani Kigoma ambapo yeye pamoja na Makatibu Wakuu wenzie, John Jingu na Christopher Kadio walikuwa Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kutathmini mnyororo wa utoaji haki jinai.
……………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum, Kigoma
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria,Profesa Sifuni Mchome amesisitiza kwamba, ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kumsingizia mtu mwingine tuhuma za ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia kwa madhumuni ya kujipatia fedha.
Ametoa maelekezo hayo siku ya jumatano wakati wa Kikao Kazi na Kamati zinazoshughulikia mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa jinsia (MTAKUWWA), baada ya kuelezwa kwamba, kuna baadhi ya wazazi katika Mkoa wa Kigoma ambao wamekuwa wakitengeneza kesi za ubakaji kama vitega uchumi.
“Niwaombe sana, mzazi au mlezi ambaye atabainika kuwa ametumia njia za uongo kutengeneza tuhuma za ubakaji na kisha kujipatia fedha, huyo anafanya jinai na anapashwa kuchukuliwa sheria kama mhalifu yeyote yule muanze kufanya hivyo.” akasisitiza Katibu Mkuu.
Maelekezo ya Katibu Mkuu Mchome, yalitokana na taarifa za kuwapo kwa baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakitengeneza matukio ya ubakaji na kasha kuamua kuyamaliza kifamili na kujipatia fedha.
WP Sakina Rashid Ndauka ambaye anasimamia Dawati la Jinsia la Polisi Kigoma Ujiji, alieleza Kikao Kazi hicho kwamba, sababu za mashauri mengi ya ubakaji kutokamilika ni kutokana na wazazi wawalalamikaji kuamua kumaliza kifamilia.
Akasema katika mashauri 56 yakiwamo ya ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni, ni mashauri 12 tu yaliyoweza kukamilika huku watuhumiwa wawili wakihukumuwa kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo Afisa Dawati huyo akasema kuna baadhi ya wazazi ambao wamegeuza matukio ya ubakaji kama kitega uchumi na kujipatia fedha.
Akatoa mfano kwamba kuna kesi moja ya tuhuma za ubakaji aliyokuwa anaifuatilia, lakini katika mahojiano na Bint aliyetuhumiwa kubakwa, bint yule aliomba azungumze na afisa dawati bila ya wazazi wake kuwapo.
“ Binti yule aliomba azungumze nami bila ya wazazi wake, na ndiyo alipokiri kwamba yeye hajabakwa isipokuwa wazazi wake wameitengeneza kesi hiyo kwa kumfundisha kwamba achukue boda boda kwenda mahali Fulani na kisha wao hutengeneza mazingira kwamba boda boda yule amembaka na kumfikisha polisi” akaeleza WP Sakina Ndauka.
Akaongeza kwamba shauri alipotaka shauri lile kulifanyia uchunguzi zaidi na hatimaye kulifikisha mahakani, wazazi wa bint yule waliomba wakalimalize wao wenyewe na huko ndipo wanapokweda kuchukua fedha.
WP Sakina amesema ameshakutana na mashauri hayo ya kuwambambikia tuhuma za ubakaji kama mara mbili hivi.
Akaongeza kwamba, licha ya familia nyingi kuamua kumaliza kifamilia matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia lakini pia kimekuwapo na visa vya walalamikaji kuwakana watuhumiwa au mashahidi kukataa kutoa ushahidi na hivyo kuleta ugumu wa ukamilishaji wa mashauri hayo kwa wakati na hivyo kujikuta na mlundikano wa majalada.
Kufuatia hali hiyo hasa ya utengenezaji wa kesi za ubakaji, ndipo Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome alipotaka wadau wa haki jinai kuanza kuwachukulia hatua wazazi watakaobainika kutengeneza kesi hizo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Christopher Kadio amewasihi wazee kutimiza wajibu wao kwa kutoa taarifa kuhusu matukio yasiyo ya kawaida yanayoendelea katika jamii zao.
Amema wazee wa nchi hii bado wanasauti na wanapaswa kuzipaza sauti hizo dhidi ya maovu yanayoendelea katika jamii.
Katibu Mkuu Kadio akabainisha kwamba kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia sababu kubwa inayotolewa ni mmonyoko wa maadili katika jamii kuwa mkubwa sana .
“ Mmomonyoko wa maadili katika jamii ni mkubwa sana, kumetokea nini? Na nyinyi wazee mpo, lakini si kwa wazee wetu tu, kila mmoja wetu ajitafakari na kuchukua hatua” akahimiza Katibu Mkuu Mambo ya Ndani.
Pia akasema serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha kuwa Polisi Jamii inashuka mpaka ngazi ya Kata. Lakini akasema huduma hiyo haitakuwa na faida ikiwa jamii hazitatoa ushirikiano ili kupunguza uhalifu na ukatili katika jamii.