…………………………………………………..
Na Joseph Lyimo
IKIWA mwezi Oktoba Kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya mtoto wa kike jamii imetakiwa kutoa nafasi na kuwapa kipaumbele watoto wa kike kwani hufanya maendeleo makubwa pindi wakiaminiwa.
Wadau wa mbalimbali wa maendeleo wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, wameitaka jamii kuwapa kipaumbele watoto wa kike katika nyanja mbalimbali ili iweze kuwaamini watoto hao na kusaidia kupatikana kwa wataalam watakaolitumikia Taifa kwa weledi.
Wadau hao wa maendeleo wameyasema hayo wakati wakizungumzia juu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yanayofanyika kila mwaka mwezi Oktoba.
Mkazi wa Mtaa wa Ngarenaro mjini Babati, Winfrida Jonas amesema jamii ikiwekeza kwa mtoto wa kike kuanzia miaka minne watoto wakiwa chekechea itwasaidia kujua haki zao na kuepuka kufanyiwa ukatili ambao unaweza kukatisha ndoto zao.
Amesema watoto wengi wa kike wanakosea au kupoteza ndoto zao kwasababu ya kukosa msingi toka wakiwa watoto wachanga ambapo alitoa mfano kuwa mzazi anaanza kwenda kunywa pombe akiwa na mtoto wa miaka miwili hivyo na mtoto akikua anajifunza hilo.
Mkazi wa mtaa wa Nangara, Hassan Ally amesema jamii inatakiwa kubadilika na kumthamini mtoto wa kike kwa kuwa yuko sawa na mtoto wa kiume.
“Mimi huwa nashangaa kuona mtoto wa miaka mitano anachungishwa ng’ombe kila siku na kuambiwa asubiri akue aolewe wakati mtoto wa kiume akipewa nafasi ya kusoma na anapewa urithi,” amesema Ally.
Ameishauri serikali kutunga sheria kali dhidi ya watu wanaodhalilisha watoto wa kike na kuwanyima nafasi za kupata elimu.
Mkazi mtaa wa Negamsi, Peter Mollel amesema jamii ya wafugaji hasa wamasai wapo watu wanachumbia mpaka mimba wakiamini watoto wa kike ni wakuolewa tu.
Mollel ameyapongeza mashirika ya haki za binadamu ambayo yamekuwa yakitoa elimu kwa kuwapa uelewa ambao umeanza kuzaa matunda na kuleta muamko wa wafugaji kuanza kusomesha watoto wa kike.
Ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Mathias Focus amekiri kuwepo kwa vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike huku akihimiza wazazi kuwatunza watoto wa kike sawa na watoto wa kiume.
Focus amesema siku ya mtoto wa kike huadhimishwa kimataifa hivyo ni sahihi kwa kuwa inasaidia kuwakumbusha watoto wa kike haki zao.
“Poa inasaidia kujitambua ili wasiendelee kuburuzwa na watu ambao wanakumbatia mfumo dume,” amesema Focus.
Amewataka wananchi kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto wa kike ili kuvikomesha kwa kuwafikisha mahakamani wahusika na siyo kuvifumbia macho kwa kumalizana kienyeji.