Mwenyekiti wa Bodi ya REPSSI Tanzania, Jeanne Ndyetabura akizungumza katika Jukwaa la Sita la kuhusu msaada wa kisaikolojia kwa watoto..
Watanzania wanaoshiriki Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Kisaikolojia kwa njia wa mtandao
Balozi wa Vijana anaye iwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Faudhia Kitenge, mmoja wa washiriki wa Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Kisaikolojia kwa Watoto..
Mkurugenzi wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala akizungumza
Tumaini Godwin, Dar es Salaam.
Tanzania imekuwa kati ya nchi 13 za Afrika zinazoshiriki Jukwaa la sita la Msaada wa Kisaikolojia hasa kwa watoto (PSS).
Jukwaa hilo limeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Malezi na Makuzi ya Watoto la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI).
Miaka ya nyuma jukwaa hilo lilikuwa linawakutanisha wadau wake kwenye nchi moja, lakini kutokana na athari za Uviko – 19, kila nchi imeshiriki kupitia kwenye mtandao ya kijamii huku Msumbiji ikiwa mwenyeji.
Akifungua jukwaa hilo leo Octoba 13, 2021, Mwenyekiti wa Bodi ya REPSSI Tanzania, Jeanne Ndyetabura amesema hata kama mtoto atapewa huduma za kijamii baada ya kukumbana na changamoto bado anahitaji msaada wa kisaikolojia na huduma ya afya ya akili.
“Ni Jukwaa linalotia ufumbuzi wa changamoto za watoto na kupanga mikakati ya namna ya kuwasaidia hasa kwenye eneo la msaada wa kisaikolojia na na afya ya akili,” anasema Ndyetabura.
Awali Mkurugenzi wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala alisema teknolojia imesaidia kufanyika kwa mkutano huo ambao isingekuwepo ungeahirishwa.
“Kwa hiyo Uviko – 19 ni changamoto, hata tunashukuru teknolojia nchi yetu inashiriki na hapa Tanzania wadau wote wakiwamo maafisa ustawi wa jamii wanakutana Hoteli ya Ramada,” amesema.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO), Epheta Msiga mkutano huo unafaida kwa wanaotoa huduma za msaada wa kisaikolojia na afya ya akili kwa watoto.
“Ili kujenga taifa lenye afya baadae na katika kusimamia makuzi ya watoto lazima msaada wa kisaikolojia na afya ya akili uzingatiwe, mkutano huu ni muhimu sana,” amesema Msiga.