NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
MUFTI wa Tanzania Abubakar Zuber Bin Ally Mbwana,amewataka Waumini wa Dini ya Kiislamu mkoani Mwanza na kote nchini,kudumisha amani,upendo, kulinda usalama na kudumisha ushirikiano na madhehebu mengine.
Alitoa kauli hiyo jana kwenye Hoteli ya Malaika,wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,hafla iliyohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa dini na serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Robert Gabriel.
Alisema ushirikiano kati ya Waislamu na waumini wa dini zingine mkoani Mwanza na kote nchini,una umuhimu mkubwa hivyo waendelee kushirikiana kudumisha amani,kulinda usalama,kudumisha upendo na kuepuka mifarakano ya kidini.
Mufti huyo wa Tanzania,alisema mafanikio yoyote ya serikali ni ya Watanzania wote na taifa letu, yanatokana na ushirikiano na uhusiano mzuri wa wananchi wake wenye imani tofauti na dini mbalimbali, wanaoshirikiana kwa mambo mengi.
“Mwali huwa hasemi,ninawashukuru kwa dhifa hii ya kuthibitisha ukarimu wenu watu wa Mwanza,dini zetu zitasimama kuwaongoza watu kiroho na kuwaelekeza waumini wetu,pia ibada kufanyika vizuri ni pale nchi inapokuwa salama na yenye utulivu,”alisema Mufti.
Aidha aliwataka viongozi wa serikali kufahamu daraja lao la uongozi na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu awaepushie balaa,chuki na husuda watekeleze majukumu yao kwa haki na uadilifu.
Kwa mujibu wa Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hassan Kabeke, Mufti Abubakar Zuberi Mbwana,alikuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua,kufungua na kuhamasisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na waumini wa dini hiyo katika mikoa ya Katavi na Tabora.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,Askofu.Dk. Charles Sekelwa, alisema ni fahari sana kwa utamaduni wa Mwanza kuondokana na fikra za kidini,utamaduni ulioendelezwa na Sheikhe Hassan Kabeke.
Alisema vurugu za Waislamu na Wakristo za nani achinje nusura ziliingize taifa kwenye vita mbaya ya kiimani lakini leo haziwezi kusikika mkoani humu kwani Mwislamu anayetaka kuleta chokochoko au Mkristo,wamejiwekea utaratibu na mfumo wa kuzishughulikia na kuzidhibiti.
“Tunapotembelewa na viongozi wakuu wa dini na kupata nasaha zao tunafarijika na tunaamini sauti zao ni sauti ya Mungu,sisi hapa Mwanza tumeunganishwa na salamu yetu ambayo mwanzo ilitaka kutufarakanisha na kututenganisha sababu ya kuchinja, vurugu ambazo zilimalizika kwa amani na ndio chanzo cha kuundwa kwa kamati ya amani Mkoa wa Mwanza,”alisema Askofu,Dk.Sekelwa.
Awali,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi Robert Gabriel,alisema Mufti Mbwana,ni heshima kubwa kumpokea Mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu anayewaongoza Watanzania wa dini ya kiislamu na taasisi zake,amekuwa mastari wa mbele kwenye vita ya ugonjwa wa Covid-19.
“Kuwepo kwako hapa leo tunakushukuru kwa kazi nzuri ya vita ya Covid-19 kwa kuhamasisha watu kuchanja,kiu yetu ni kupata dua zako na wananchi wakiwemo waumini wa kiislamu wana kiu ya kupata baraka za Mungu ulizotembea nazo na sisi Mwanza tufurahi tumeuona mkono wa Mungu,”alisema.