Home Mchanganyiko WASHAURI MAKOSA YA KUJIFANYA AFISA TAKUKURU NA RUSHWA YA NGONO...

WASHAURI MAKOSA YA KUJIFANYA AFISA TAKUKURU NA RUSHWA YA NGONO YAONDOLEWE KATIKA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI

0

Mwenyekiti wa Jukwaa la  Haki Jinai  Mwendesha Mashtaka Mkoa wa  Kigoma,  Riziki Matitu akiwasilisha Taarifa ya Jukwaa wakati wa Mkutano wa Kikao Kazi kilichoongozwa na Profesa Sifuni Mchome Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, wengine katika picha ni wajumbe wa Jukwaa hilo.

Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome akizungumza  katika kikao kazi  kilichowahusisha Jukwaa la Haki Jinai Mkoa  wa Kigoma na Jukwaa la kupinga ukatili wa Kijinsia uliofanyika  siku ya Jumatano  Mkoani Kigoma,  wengine katika picha ni  Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto John Jingu na  Chritopher Kidau, Katibu Mkuu  Wizara ya Mambo ya Ndani.

***************************

Na Mwandishi Maalum- Kigoma

Wajumbe wa  Jukwaa  la  Haki  Jinai Mkoa wa Kigoma,  wameishauri Serikali,  kuifanyia marekebisho  Sura ya  329 marejeo ya mwaka 2019 ili kuondoa baadhi ya makosa kuwa ya uhujumu  au kuhitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka  kufungua kesi.

Ushauri huo umetolewa   siku ya Jumatano na   Wajumbe hao wakati wa Kikao Kazi kilichoongozwa na Profesa Sifuni Mchome , Katibu Mkuu  Wizara ya Katiba na Sheria. Kikao hicho  pia kiliwashirikisha Makatibu Wakuu, John Njingu,  Katibu Mkuu  Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Christopher Kidau, Katibu Mkuu   Wizara ya Mambo ya Ndani.

Makatibu hao watatu wapo katika ziara ya kikazi  ya kutathimini  utoaji wa hakijinai , mafanikio, changamoto na hata kuzitolea ufumbuzi au uamuzi wa papo kwa papo wa    baadhi ya changamoto hizo.

Akiwasilisha Taarifa ya  Jukwaa hilo kwa Makatibu Wakuu hao,  Mwenyekiti wa Jukwaa,  Mwendesha Mashtaka Mkoa wa  Kigoma  Riziki Matitu, ameyataja baadhi ya makosa ambayo  yanahesabiwa kama uhujumu  uchumi ni  pamoja  mtu kujifanya Afisa  Takukuru na rushwa ya ngono.

“ Tunashauri na kupendekeza kwamba,  Sheria ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa Sura ya  329 marejeo ya mwaka 2019, irekebishwe ili kuondoa baadhi ya makosa kuwa ya uhujumu uchumi na au kuhitaji kibali  cha Mkurugenzi wa Mashtaka ili kufungua  Kesi. Kwa mfano kosa la kujifanya Afisa  Takukuru Kifungu cha 36 na rushwa ya ngono  kifungu cha 25” akasema Mwenyekiti wa Jukwaa. Riziki Matitu.

Pamoja na  kutaka kufanyiwa marekebisho  kwa sheria hiyo, Jukwaa la Haki Jinai ambao wajumbe wake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa, Mkuu wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa, Mkuu wa Magereza,  Mratibu wa Huduma za Kijamii na Mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha Mkoa,   limeshauri pia  Sheria ya kulinda  mashahidi na watoa taarifa  Na 20 ya mwaka2015 itengenezewe kanuni.

Jukwaa hilo  linataka kutungwa kwa kanuni hizo  kwa kile walichosema kumekuwapo na changamoto kubwa zinazowakabili   mashahidi na watoa taarifa  ikiwamo  kutishiwa maisha au  kutojitokeza kutoa ushahidi kwa kuhofia maisha yao  na hata kuugeuka ushahidi waliokwisha kuutoa  kutokana na vitisho wanavyopewa.

“Mhe. Katibu Mkuu  sisi Jukwa la Haki Jinai,  tunapendekeza pia  Sheria ya kulinda mashahidi na watoa taarifa Na 20 ya mwaka 2013 itengenezewe kanuni  kama ilivyoainishwa  kwenye kifungu cha 15 cha sheria hiyo ili kuelekeza jinsi ya kutoa ulinzi kwa mashahidi au watoa taarifa wanaopata madhira kwa kushirikiana na  vyombo vya uchunguzi au mashtaka”

Katika kupunguza msongamano  wa mahabusu na wafungwa katika  magereza,  Wajumbe wa  Jukwaa  pia wameshauri haja na umuhimu wa  matumizi wa adhabu mbadala kwa baadhi ya makosa na wakataka elimu zaidi itolewa kwa Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Mawakili na Jamii   ili iwe tayari kupokea adhabu hiyo bila kujenga  viashiria vya rushwa ndani yake.

Wakatoa mfano kwamba,  katika  tathmini iliyofanywa mwezi Machi Mwaka huu na  Mahakama Kuu Kanda ya  Kigoma,  iligundua kwamba kati ya washtakiwa  182 waliofungwa gerezani  kifungo kisichozidi  miaka mitatu ambao wangeweza kupewa  adhabu ya huduma  kwa jamii na hivyo ingesaidia sana kupunguza msongamano magerezani.

Hata hivyo jukwa hilo limesema  adhabu  za fine na  huduma za jamii zipewe kipaumbele, isipokuwa uhalifu wa kutumia nguvu,  unyanyanyi, uhaini, ugaidi na  mauaji” wakasema wajumbe wa  Jukwaa.

Akijibu mapendekezo nayo  na mengine yaliyowasilishwa  katika Kikao Kazi hiyo,  Katibu Mkuu  Profesa  Sifuni Mchome, amesema.“ Katika hili la sheria ya TAKUKURU nisema tu mchakato wa mapitio ya sheria  hiyo unaendelea vizuri, kwa sababu kuna baadhi ya makosa yasingekuwa  na hoja ya  kuwa katika sheria hii. Kuna baadhi ya  makosa  yakiwamo  kwa mfano ni  mali au fedha ya thamani gani inapashwa kuingia katika kosa  la uhujumu uchumi,  na mengine mengi  tunayaangalia, si muda mrefu kazi hii itakuwa imekamilika” akabainisha Katibu  Mkuu Mchome.

Kuhusu  kutungwa kwa kanuni za  kuwalinda  mashahidi na watoa taarifa, Katibu Mkuu mchome amewahakikishia wadau hao wa Hakijinai kwamba kanuni hizo zitakuwa zimekamilika ifikapo mwishoni mwa   mwaka huu.

Aidha Katibu Mkuu Mchome amesema,  Mamlaka ya  Mwendesha Mashtaka sasa yameshushwa katika ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa baadhi ya mashauri ili kupunguza uchelewesaji wa mashauri. Akasisitiza haja na umuhimu wa  Taasisi zote zinazohusika na  utoahi haki kufanya kazi  kwa ushirikiano  huku zijichukua tahadhari ya kutoingilia wajibu na mamlaka ya Taasisi nyingine.

Kuhusu  wafungwa kukosa sifa za udhamini, Profesa Mchome amebainisha kwamba  kazi imeaanza ya  kufanyika kuhuisha  mfumo wa Polisi, NIDA na  Mahakama ili  kurahisisha upatikanaji wa dhamana kwa watuhumiwa  ambao makosa yao yanastahili dhamana.

Wakiwa Mkoani  Kigoma, Makatibu Wakuu hao  pia wamekuwa na  mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Tobias Andegenye,  Vikao  Kazi na  Wajumbe wa Kamati ya  MTAKUWA ya Manispaa ya Kigoma/ Ujiji,Wajumbe  wa Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi na pia walitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Gereza la  Kigoma Mjini ( Bangwe) na Kambi ya Wazee Kibirizi.

Wakiwa katika Gereza la Bangwe, Makatibu Wakuu hao walitoa fursa  kwa wafungwa na mahabusu kutoa kero zao.

 Baadhi ya kero zilizowasilishwa na  mahabusu na wafungwa hao ni pamoja na kutokuwa na bima ya afya na hivyo kuiomba serikali  kuwafikiria.

Aidha wafungwa hao wameomba kupatiwa mablanketi  na magodoro.

Gereza la  Bangwe  ambalo limejengwa mwaka 1938 likiwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 69 sasa linauwezo wa kuhudumia wafungwa na mahabusu 198 baada ya kupanuliwa na kwamba halina msongamano.

Kwa upande wa huduma za Afya, Wafungwa  71 wamechanjwa kwa hiari chango ya Covid- 19  huku  maafisa na askari 6 wamechanjwa kwa hiari yao

Makatibu Wakuu hao Ijumaa   watakuwa   Mkoani wa Kagera.