WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya watendaji na waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu,wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu,akimsikiliza Naibu Waziri Dkt. Festo Ndugage,wakati akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshugulikia Afya Dkt. Grace Magembe,akielezea namna utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu,amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia kikamilivu miradi mbalimbali kwa fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani IMF iliyolenga katika mapambano dhidi ya UVIKO 19 hapa nchini.
Hayo ameyasema leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ummy amesema kuwa Fedha za mkopo kutoka shirika la fedha duniani IMF, kiasi cha Sh. Trioni 1.3 zinahitaji usimamizi mzuri na miradi ijengwe kulingana na ubora na miradi iendane kulingana na thamani ya fedha.
Ummy amesema kuwa TAMISEMI katika mkopo huo imeidhinishiwa kiasi cha Sh. bilioni 535.6 sawa na asilimia 41.1 ya fedha zote na zitatumika katika kutekeleza vipaumbele vyote.
“Nitumie fursa hii kutoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia pamoja na kuunda Kamati ya Mkoa ya uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi husika na kuhakikisha kwamba taarifa za utekelezaji wa miradi hii zinawasilishwa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila baada ya wiki mbili.”amesema Ummy
“Naelekeza kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaanza ndani ya wiki mbili mara baada ya fedha kupokelewa miradi ya ujenzi wa madarasa ikamilike ifikapo desemba 15, mwaka huu na ile mingine ikamilike ifikapo Aprili 30, 2022,.”amesisitiza
Aidha amesema,katika utekelezaji wa miradi hiyo Halmashauri zinaweza kutumia wakandarasi wa ndani au utaratibu wa “force account”
Aidha, amesema kuwa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo hakuna Mkuu wa Mkoa wala wilaya ambaye ataruhusiwa kuondoka katika eneo lake la kazi.
“Mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya wote wanatakiwa kubaki katika eneo lao la kazi wakati wote wa utekelezaji wa mradi hadi ukamilike na atakaye toka ni yule tuu ambaye atapatiwa kibari na Rais, Makamu wa Rais au Waziri mkuu na siyo vinginevyo”amesisitiza Ummy
Amesema kuwa kiasai cha Bilioni 302.7 zitatumika katika sekta ya elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa 12,000 vya sekondari ili kuwezesha wanafunzi wote kuanaza masomo kwa wakati mmoja.
“Mradi huu utatusaidia kuondoa masula ya second selection kwasababu yatakuwepo madarasa ya kutosha pamoja na madawati”amesema Ummy
Amesema kuwa Serikali imepanga kujenga vyumba vya madarasa 12,000 vitakavyogharimu Shilingi bilioni 240 katika shule za sekondari katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaojiunga mwezi Januari, 2022.
“Ujenzi wa idadi ya vyumba vya madarasa haya unatokana na mahitaji kulingana na idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022, maoteo ya ufaulu kitaifa yanatofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kwa wastani wa ufaulu wa kitaifa wa asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani darasa la saba 2021,
“Hivyo wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2022 ni 1,022,936 mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 20,535 ambayo hailingani na idadi ya vyumba vya madarasa 8,535 vitakavyoachwa wazi na wanafunzi 422,403 wa kidato cha nne watakaofanya mtihani mwezi Novemba, 2021. Hivyo, uhaba wa vyumba vya madarasa 12,000.”