Home Siasa CCM YAELEKEZA VIONGOZI WAKE KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI ZILIZOTOLEWA NA IMF

CCM YAELEKEZA VIONGOZI WAKE KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI ZILIZOTOLEWA NA IMF

0

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapindunzi CCM Taifa, Itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma.

…………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewasisitizia viongozi na watendaji wenye dhamana kuanzia serikali kuu hadi kwenye halmashauri za wilaya kuhakikisha  fedha zilizotolewa za  mkopo wa masharti nafuu kutoka  Shirika la fedha  la kimataifa (IMF) zinakwenda kutekeleza miradi iliyokusudiwa ili kuleta matokeo yaliyolengwa kwa ustawi wa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 12,2021 Jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapindunzi CCM Taifa, Itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.

Shaka amesema fedha hizi na zingine zote zinatolewa na serikali kwenda kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo,CCM haitakubali kuona fedha za umma zikitumiwa visivyo na kuibebesha lawama Chama ambacho ndicho kilichopewa dhamana na wananchi ya kuunda na kuongoza serikali.

Aidha,Shaka  amesema endapo fedha hizo zitatumika na  mtu atakayedhibitika kuhusika   na ukwapuaji wa fedha hizo hawatasita kuielekeza Serikali kumfikisha muhusika mbele ya vyombo vya sheria.

Shaka amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan chini ya serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha majadiliano yaliyopelekea kupata fedha hizo kwa matumizi ya mazingira ya nchi badala ya kubanwa katika maeneo ya ununuzi wa chanjo za Uviko-19 pekee.

Amesema Rais Samia alifanya uzinduzi wa kampeni ya Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 ambayo inagharimu takribani trilioni 1.3 ikiwa ni msaada na mkopo wa masharti nafuu kutoka IMF.

Aidha Shaka ametoa wito kwa watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na Serikali yake kwa kuendeleza na kudymisha umoja,amani na mshikamano uliopo nchini ili kumpa nafasi nzuri ya kuijenga nchi.

Pia  Shaka amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kulinda tunu za Taifa na kusimamia msingi mkuu wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“ Rais Samia ameendelea kulinda na kuimarisha utawala wa sheria,demokrasia ya vyama vingi,usawa ,haki za binadamu,nchi isiyofungamana na dini yoyote ,kupambana na unyanyasaji na udhalilishaji wa aina zote,”alisema

Wakati huo huo Chama  cha Mapinduzi CCM,kimetoa pongeza kwa Chama cha ACT Wazalendo kwa ushindi katika jimbo la Konde wilaya ya Micheweni  mkoa wa kaskazini Pemba kwa ushindi waliopata katikauchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Pia Chama hicho kimewashukuru na kuwapongeza kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga kwa kumchagua Emanuel  Cherehani kwa kushinda katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo na kuibuka kidedea kwa kura 103,357 sawa na asilimia 96.6

Hata hivyo Shaka ,amesema  Chama chao kinatoa pongezi kwa Chama cha Act  Wazalendo kwa ushindi uliopata kwani hiyo ndio maana halisi ya dhana ya siasa safi na demokrasia ya kweli.

Amesema  pia wanashukuru wananchi wa kata tatu za Tanzania bara ambazo ni Neruma (Bunda,Mara),Lyowa(Kalambo,Katavi) na Vumilia (Urambo,Tabora ) kwa kuipa ushindi mkubwa chao chao .

Shaka amesema  kumalizika kwa uchaguzi huo mdogo kwa amani na utulivu ni jambo la kujivunia kwani wanaendelea kujifunza mambo kadhaa ambayo yanajenga katika umoja na mshikamano kwao.