Katika kusheherekea Wiki ya Huduma kwa Wateja, wanachama wa PSSSF mkoani Tanga wamepongeza huduma wanayopatiwa siku kwa siku kuwa ni ya haraka na yenye kuzingatia weledi.
Akiongea kwa niaba ya wastaafu waliokuja kupatiwa huduma katika Ofisi za PSSSF Tanga, mstaafu Mwl. Valentine Ngoiya Adriano alisema “huduma za ofisi ya PSSSF Tanga ni zenye kuzingatia weledi na uharaka ambayo inatusaida kupata majibu ya madai yetu kwa wakati”
Akielezea ni nini anachotegemea kama mteja na mwanachama wa PSSSF, Mwl Valentino, alisema baada ya kutumikia Serikali kwa kipindi kirefu anategemea kupata huduma kama mteja anayethaminiwa kwa kujali utumishi uliotukuta ambao ametumikia katika Taifa. Alitoa rai kwa uongozi wa Mfuko wa PSSSF kutoa elimu juu ya mafao ili wastaafu waweze kuwa na matumizi sahihi ya kiinua mgongo ambacho wamepata katika uzee wao. “Wastaafu wengi hupoteza pesa ambazo wamepata kama kiinua mgongo kwa sababu ya kuingia katika biashara ambazo kimsingi haziendani na umri wao na hivyo kupoteza pesa na matokea yake kuishi maisha ya uzee ambayo hayana staha”.
Katika salamu zake kwenye kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja ambayo ilianza Oktoba 4, 2021 na kufikia kilele Oktoba 8, 2021 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo C.P.A Hosea Kashimba alisema PSSSF inawahakikishia Wanachama wake na Jamii kwa ujumla kuwa itaendelea kutoka huduma Bora wakati wote.
“ Ujumbe wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ni nguvu ya Huduma yaani Power of Service, sisi tutajikita katika kuonesha ni namna Gani tutajenga imaani kwa Wateja wetu kwa kutumia teknolojia tuliyonayo kumaliza kero zao,” alisema C.P.A Kashimba na kuongeza……kutumia mtandao wa Ofisi zetu kupunguza muda ambao mwanachama wetu angefika kutatuliwa matatizo yake, kutasaidia sana kupunguza kero kwa Wanachama wetu.” Alifafanua.
Aliahidi kuendelea kwa ukarimu wa wafanyakazi wa PSSSF kuwa watawahudumia Wanachama viziri wafikapo kwenye Ofisi za Mfuko na watatoka wameridhika.
Akiongea na wanachama waliokuja kupata huduma katika ofisi za PSSSF Tanga, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Bi. Laila Maghimbi, alisema katika Wiki ya Hduma kwa Wateja PSSSF inasheherekea kazi kubwa inayofanywa na watumishi wa PSSSF ya kuangalia na kulinda maslahi ya wanachama. “Ni muda pia tunapata kama watumishi wa Mfuko kuangalia kwa undani namna ambayo tunahudumia wanachama wetu, kuboresha huduma zetu na kuona ni namna gani tunaweza kuboresha kwa kutoa huduma bora zaidi.”
Akiongea na wanachama kwa nyakati tofauti, Meneja wa Uhusioano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe, alisema muda huu unatupatia nafasi nzuri ya kujiuliza mteja wetu anataka nini? “Hii inatusaidia kuendeleza utamaduni wa huduma kwa mteja na matokea yake ni kwamba utamaduni huu polepole unaingia katika utamaduni wa utendaji kazi wa watumishi wa Mfuko.
Alimalizia kwa kusema huduma iliyotukuka kwa wanachama wetu ni haki ya kila mwanachama. “Bila wanachama hakuna PSSSF, hivyo basi kila mmoja wetu ana wajibu wa kutoa huduma bora kwa maslahi mapana ya Mfuko wetu na wanachama.
Wiki ya Huduma kwa Wateja ni siku inayosheherekewa na mashirika na taasisi kimataifa duniani kote inayosisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa huduma kwa wateja kwa kukuza uimara wa taasisi.