Makamu Mkuu wa Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinaty Kamuhabwa akizunguza katika mkutano wa wafanyakazi wa Muhimbili uliofanyika leo hospitalini hapo kutathimini athari za ugonjwa wa UVIKO-19 na kuhamasishana kwa ajili ya kuchukua tahadhari ikiwani pamoja na kuchanja.
Wataalamu wa afya wa MUHAS wakiwa katika kikao cha tathimini ya chanjo ya UVIKO-19
………………………………………….
Tunayo majukumu mbalimbali ya kazi ambayo yanatungojea lakini sisi kama wataalam tunayo kila sababu na umuhimu wa kutenga muda na kuhudhuria mkutano huu ambao ni hatua moja ya mafanikio, madhumuni, na malengo madhubuti ya kuhakikisha tunakaa pamoja na kujadili changamoto mbalimali tulizopitia katika mapambano ya ugonjwa wa UVIKO -19 toka ulipoingia nchini mwetu
Mkutano huu ni muhimu sana na lengo la kuandaa mkutano kwa wafanyakazi wote ni kujadiliana kwa pamoja jinsi la kukabiliana na janga la UVIKO-19 linaloikabili nchi yetu na dunia kwa ujumla, Nitoe shukrani zangu za dhati kwenu nyote kwa niaba ya Menejimenti ya Chuo kwa kuitikia wito na kuhudhuria mkutano huu.
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba yake katika mkutano huo Makamu Mkuu wa Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinaty Kamuhabwa amesema takribani miaka miwili Tanzania kama nchi nyingine nyingi duniani kote, imekuwa ikikabiliwa na janga la UVIKO-19. Kama tunavyofahamu watu wengi wamepoteza maisha kutokana na janga hili.
“Sidhani kama kuna mtu hapa hajapoteza ndugu, jamaa, rafiki au mtu unayemfahamu kutokana na janga hili na wengi wetu ni zaidi ya mmoja. Vile vile sisi kama wafanyakazi bado tuna majonzi ya kupoteza baadhi ya wafanyakazi wenzetu kutokana na janga hilo ambapo wengi wetu tumepitia mateso makubwa ya kuugua au kuuguza kwa muda mrefu mgojwa wa UVIKO-19.” Amesema Kamuhabwa
Aidha amefafaniua kuwa hapa nchini kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na janga hili ambayo inaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kubwa katika mikakati hiyo ni namna mbalimbali za kujikinga ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano na pia kuvaa barakoa unapokuwa kwenye mikusanyiko ya mtu zaidi ya mmoja.
“ Ninatambua kabisa mambo hayo yote tuyajua na tumekuwa tukiyazingatia kwa kiasi fulani, ni dhahiri hatuwezi kusema au kujisifu kwamba tumekuwa tukiyatekeleza hayo yote kwa uaminifu kabisa, kwani tunajua tabia au mazoea yanachukua muda kubadilika,”. Amesema Kamuhabwa
Kutokana na hilo basi hatuna budi kukumbushana mara kwa mara ili kwa pamoja tuweze kushinda na kudhibiti kwa kiasi kikubwa maambukizi mapya ya UVIKO -19 hapa chuoni na nchini kwa ujumla.
Lengo kuu la mkutano huu ni kuhamasishana juu ya jinsi ya kujikinga na janga la COVID-19 ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo kwenye masuala ya chanjo. Kama tunavyofahamu kumekuwa na malumbano mengi kwenye masuala ya chanjo ya UVIKO-19 hapa nchini na duania kwa ujumla.
Ameeleza kwamba malumbano hayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kutokuwa na taarifa sahihi zinazohusiana na chanjo kutoka kwa watu sahihi.
“Watu wamekuwa wakipata taarifa hizo kwenye mtandao ambapo vyanzo cha taarifa hizo sio vya kuaminika (unreliable sources) kwa hivyo kumekuwa na upotoshaji mwingi ambao umewafanya watu wengine kukosa imani na chanjo”. Amesema Kamuhabwa.
Hivyo basi kama Chuo kilichojikita kwenye masuala ya afya, tuna bahati ya kuwa na maguru wa masuala ya chanjo nchini. Ndio maana tumeona ni muhimu kuwa na mkutano huu kwa wafanyakazi wote ili tuweze kutumia hazina tuliyonayo kuelekezana na kujadiliana kuhusiana na masuala ya kujikinga na UVIKO -19 ikiwa ni pamoja masuala ya chanjo.
Ni vema tukapata nafasi ya kusikia kutoka kwa wenzetu ambao wana uzoefu mkubwa na pia wamebobea kwenye masuala hayo. Tupate na nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yamekuwa yakitutatiza ili kufanya maamuzi yenye ufahamu (Informed Decision).
Katika hilo pia kulikuwa na kituo kidogo Chuoni hapo ili kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa wale watakaofanya maamuzi hayo ya kuchanja baada ya kupata elimu ya chanjo.
Nawashukuru watoa mada walioongozwa na Mtaalamu mbobezi wa masuala ya chanjo, Prof. Eligius Lyamuya, kwa kutoa muda wao kutekeleza jukumu hilo na kwa utayari mkubwa sana.
Amewataja wataalam wengine ambao walitoa mada katika jopo la wawezeshaji ni pamoja na Prof. Raphael Sangeda, Dr. Mariam Amour, Dr. Pascal Ruggajo, Dr. Frank Msafiri na Bw. Emmanuel Sumari. Kwa niaba ya manejimenti ya Chuo ninasema asanteni sana na tuna Imani mtayaongoza majadiliano haya kwa uweledi mkubwa na lugha rahisi ya kuweza kufikisha ujumbe wa pamoja kwa wafanyakazi wote.