…………………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA, UKEREWE
WANANCHI wa Kitongoji cha Kisiwa cha Gana,Kijiji cha Kamasi,Kata ya Ilangala, Wilaya ya Ukerewe, wajitokeza kwa wingi kupata elimu ya chanjo ya Uviko-19 iliyotolewa na timu ya wataalamu wa Afya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali. Denis Mwila.
“Eneo hili la Gana lina muingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za kiuchumi, ili kuwa salama na Uviko-19 ni vizuri kuchanja na chanjo zipo za kutosha, ni salama na hazia madhara, ukiachilia mbali maudhi madogo madogo,”alisema Kanali Mwila.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Dk.Getera Nyangi,akitoa elimu ya ugonjwa wa Uviko-19 aliwatoa hofu wananchi hao na kuwataka kupuuza maneno yasiyo kuwa na uthibitisho juu ya chanjo hiyo ambayo imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya.
Aliyataja makundi na watu wenye sifa za kupata chanjo hiyo ni pamoja na wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea na sio kwa watu wenye umri mkubwa tu kwa sababu ugonjwa hauchagui.
“Hadi sasa takribani watu 2,064 wilayani Ukerewe na hakuna hata mmoja aliyeripoti kupata changamoto yoyote ya kiafya inayotokana na chanjo, hivyo tuchanje kwa afya zetu,” alisema Dk. Nyangi.
Aidha wananchi wa kitongoji cha Gana waliojitokeza kwa wingi kuchanja walipata fursa ya kuuliza maswali yanayowatatiza na kupatiwa majibu ya kitaalamu.