Na. Lillian Shirima: MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeongeza kasi ya kutumia njia mbalimbali za kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa Uviko-19 ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma ya chanjo nchini kote ili kuzuia vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Afisa Program na Mratibu wa Kamati ya Maudhui, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana Saimon Nzilibili amesema hayo Wilayani Bagamoyo katika Kikao Kazi kilichowakutanisha Wawakilishi wa Viongozi wa Dini kutoka Madhehebu yote.
Washiriki wengine ni kutoka Taasisi za Kiserikali na Wadau wa Maendeleo na Huduma za Afya kutoka WHO, UNICEF na Family Heath International (FHI) ambao kwa pamoja wamekutana kuandaa nyenzo maalum zitakazotumiwa na viongozi wa Dini nchini kutoa taarifa kwa waumini wa dini zote kuhusu ugonjwa wa Uviko-19 upatikanaji wa chanjo kama njia ya kujikinga maabukizi ya ugonjwa huo.
“tunaendelea kuhakikisha makundi mbalimbali ya watanzania yanafikiwa kwa kutumia mbinu tofauti, matangazo ya radio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii na sasa hii nyenzo (bango kitita) inayoandaliwa ni kwaajili ya viongozi wa Dini’.
Aidha, amesema, nyenzo za viongozi wa Dini zitatumika katika mpango maalum wa utakaotumiwa na viongozi hao kwa kipindi cha majuma manne mfululizo na baadaye kujirudia kila utakapokamilika ili kusaidia waamini kuelewa kwa ufasaha ugonjwa wa Uviko-19 na kupata taarifa mbalimbali zinazoeleza faida ya chanjo kwa ujumla.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Bw. Saimon amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwafikia wananchi mahali walipo hivyo kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mpango shirikishi na harakishi unaolenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kupokea huduma ya chanjo ambayo inazuia vifo vitokanavyo na Uviko-19.
Mpango huo umewaleta wakufunzi zaidi ya 200 ambao tayari wapo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Halmashauri zake wakiendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii na kuwahamasisha waweze kutambua madhara yatokanayo na Uviko-19 na hatimaye kuamua kwa hiari kupata chanjo kama wanavyoelekeza wataalamu wa afya.
‘Ni vema jamii ikaitikia na kushika mafundisho ya wataalamu wetu na maelekezo yanayotolewa na serikali, kila mmoja wetu ahamasike na kuelewa umuhimu wa kupata chanjo ili tubaki kuwa taifa salama’.
Naye Mchungaji Basilisa Ndonde kutoka Kanisa la Pentekoste ameishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo viongozi wa dini na kuwashirikisha katika hatua za kutafuta njia bora ya kufikisha taarifa sahihi kwa jamii kuhusu ugonjwa wa uviko-19 na namna ya kujikinga ikiwepo kupata chanjo kama inavyoshauriwa na wataalam.
Amesema, mbali na kuwa viongozi wa dini wanao wigo mpana wa kutoa huduma kiroho hadi kwenye maeneo yasiyofikika kirahisi vilevile wanao uelewa mkubwa wa mila na desturi za waumini wao kwakuwa wanaishi katika mazingira yao.
‘tunaishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa viongozi wa dini na kutushirikisha kuandaa material (nyenzo) tutakazotumia kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya chanjo ya corona na faida zake , sisi ndio tunaishi nao, tunawafahamu waumini wetu’.
Amesema, mara nyingi viongozi wa dini wanaulizwa maswali magumu na waumini wa madhehebu mbalimbali hivyo nyenzo wanazoandaa na mafunzo wanayopatiwa yatawasaidia kukuza uelewa wa pamoja kuhusu uviko-19 na kuondoa sintofahamu iliyopo miongoni mwa jamii lakini pia kuepusha upotoshaji wa taarifa za uviko-19.
Kwa upande wake Katibu wa Vijana wa Kiislamu, Baraza Kuu la Waislam Taifa (BAKWATA), Bw. Othman Zuberi amesema, bado kuna umuhimu mkubwa wa viongozi wakuu hususani wanaoishi na jamii kuanzia ngazi ya kijiji kuhamasisha watu kupata chanjo kwasababu wao ndio mfano wa kuingwa na wanakijiji.
Akitoa mfano wa Siku ya Uzinduzi wa chanjo ya Uviko-19 julai 28 mwaka huu, Bwana Othman Zuberi amesema kitendo cha Viongozi Wakuu wa Halmashauri Kuu ya Bakwata kupata chanjo kimeamsha ari kwa waumini wa dini hiyo kupata chanjo, hivyo amewasihi vijana kukubali chanjo kwani vijana ni miongoni mwa makundi yanayoathirika na kusababisha taifa kupoteza nguvu kazi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, ametoa ushauri kwamba taarifa za upotoshwaji wa chanjo zisiachwe ziendelee kusambaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii isipokuwa zipatiwe majibu sahihi na kwa wakati maana Serikali inao wataalamu waliobobea katika sekta ya afya.
‘Wapotoshaji ni wengi, wanasema wao, wanasikika wao mitandaoni na maeneo mengine ambayo yanapeleka taarifa kwa jamii yametawaliwa na wao., wataalam wanayo maelezo mazuri ya maswali yanayoulizwana jamii, waenelee kutoa nufafanuzi kila wakati’.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kupambana na janga la Uviko-19 kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupokea chanjo, kuongoza Watanzania katika zoezi la kupata chanzo na kusisitiza watu waelimishwe kuhusu madhara ya ugonjwa na faida ya chanjo ili waweze kufanya maamuzi sahihi.
Katika Mkutano Mkuu wa Viongozi wa Jumuiya za Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika Septemba 27, 2021 Jijini Dodoma Mhe. Samia Suluhu Hassan, nchini Tanzania yapo matatizo ya ugonjwa wa TB,, HIV na Malaria ambayo Serikali kwa kiasi kikubwa imepiga hatua katika kuyatatua na kwamba tatizo la Uviko-19 lililojitokeza ni tatizo kubwa linalohitaji kushughulikiwa ipasavyo.
‘..Nendeni mkalishughulikie, mtu hana mamlaka ya kukubali au kukataa kama anayo elimu, kama ana elimu ya kutosha hawezi kukataa, ……. Nendeni katoeni elimu kwa wananchi kafanyeni massive kampeni ya hili suala la uviko-19 ……
Katika historia ya dunia, chanjo zimeonesha kuwa nyenzo muhimu katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kuimarisha afya ya jamii. Hadi sasa kuna aina mbalimbali za chanjo ya ugonjwa huu kama vile Sinopharm, AstraZeneca, Jensen, Pfizer na nyinginezo
Julai Mwaka 2021, Tanzania ilipokea shehena ya kwanza ya chanjo 1,058,400 aina ya Johnson & Johnson kutoka nchini Marekani, iliyoletwa chini ya Mpango wa Shirika la Afya Duniani unajulikana kama Covax Facility ikiwa ni msaada wa kukabiliana na Uviko-19.
Chanjo hizi zinalenga kuzuia madhara yatokanayo Uviko-19 si Tanzania pekee isipokuwa duniani kwa ujumla. Hadi kufikia Julai, 2021 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limetangaza idadi ya vifo vya watu 186,411,011 duniani.
Ugonjwa wa Uviko-19 uliripotiwa kuingia nchini tarehe 16, Machi 2020 na kama zilivyo nchi nyingine ugonjwa unaendelea kuathiri mifumo ya afya, uchumi na masuala ya kijamii kusababisha na hofu kwa jamii.
Hivyo, uelimishaji wa jamii kuhusu ugonjwa wa Uviko-19, utoaji wa chanjo nchini unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19, mpango unaoelekeza matumizi ya chanjo kama mkakati wa kuzuia maambukizi zaidi. Ni vema sote tukazingatia maagizo ya wataalamu wetu na kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali yetu.