Makusanyo ya *Kodi ya ushuru wa bidhaa* yameongezeka zaidi katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita iliyopita, jambo ambalo limechangiwa na kuanzishwa kwa Stempu za Kodi za Elektroniki (ETS).
Serikali ilitangaza mpango wa kuanzisha mfumo wa ETS Juni 2018 na awamu ya kwanza ya mradi ilifanyika Januari 15, 2019 ambapo stempu ziliwekwa kwenye kampuni zinazozalisha bia, mvinyo na pombe.
Awamu ya pili ya mradi huo ilianza Agosti 1, 2019 wakati stempu za ETS zilibandikwa juu ya maji yenye ladha na vinywaji vingine visivyo vya pombe, kama vile vya *kuchochea nguvu mwilini* na vinywaji vya malt na soda.
Awamu ya tatu, ambayo ilijumuisha kusajili stempu za elektroniki kwenye juisi za matunda (pamoja na mchuzi wa zabibu), juisi za mboga na maji ya kunywa ya chupa, ilianza Novemba 1, 2020.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa makusanyo ya *Kodi ya ushuru wa bidhaa* yameongezeka kwa asilimia 60 ikiwa miaka mitatu kabla ya kutolewa kwa ETS kwenye bia, mvinyo na pombe italinganishwa na kipindi kama hicho baada ya kutolewa.
“Tulikusanya Sh297.2 bilioni kama Kodi ya ushuru wa bidhaa kwenye bia, mvinyo na pombe (zote zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa nchini) katika kipindi cha miaka mitatu kabla ya Januari 15, 2019 lakini kutoka wakati huo hadi Juni 2021, kiasi hicho kiliongezeka hadi Sh476.7 bilioni,” alisema msimamizi wa mradi wa ETS kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA), Innocent Minja.
Alisema kumekuwa na viwango vya ongezeko la *Kodi ya shuru wa bidhaa* katika tarakimu mbili kutoka kwenye bidhaa zote ambazo stempu za ETS zinabandikwa.
“Ushuru wa bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bia zimepanda kwa asilimia 15 wakati ile ya vinywaji baridi imepanda kwa asilimia 29. *Kodi ya Ushuru wa bidhaa* na VAT kwenye maji ya chupa imepanda kwa karibu asilimia 156, ”alisema.
ETS inaiwezesha serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata takwimu za uzalishaji kwa wakati unaofaa kutoka kwa wazalishaji. Kwa njia hiyo, haiwezeshi tu serikali kukusanya kiwango sahihi cha kodi ya bidhaa lakini pia inazuia kuingia kwa bidhaa bandia sokoni.
Kwa mujibu wa Minja, kunaweza kuwa na nafasi ya uboreshaji zaidi katika usimamizi wa mradi huo, lakini ukweli uliowazi ni kuwa hadi sasa, faida zimeonekana hata kwa wazalishaji.
“Wakati tunazingatia maoni ya wazalishaji kuhusu hitaji la kupitia upya viwango vya ETS, tunaamini pia kuwa mradi huo umekuwa wa faida kwetu sote…. Inasaidia wazalishaji kuwa na uhakika wa kiwango chao cha uzalishaji kwa wakati halisi,” alisema. .
Kabla ya kupitishwa kwa ETS, Kodi ya ushuru wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini ulikuwa ukiwekwa kupitia stempu za karatasi ambazo TRA inasema ilikuwa rahisi kuchezewa.