NA TIGANYA VINCENT
WAKAZI wa Mkoa wa Tabora wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha za bajeti ya barabara za vijijini kwa asilimia 300 .
Shukurani hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati ziara yake katika Mnada uliopo katika Kijiji cha Mwisole wilayani Uyui akitoa elimu ya mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa chanjo ya UVIKO 19.
Amesema hapa awali Mkoa wa Tabora ulikuwa ukipata kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa mwaka lakini Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha hizo na kufikia bilioni 27 kwa mwaka.
Balozi Dkt. Batilda amesema ongezeko hilo litasaidia kuondoa kero katika maeneo korofi ambayo ni muhimu kwa ajili wakulima kupata huduma mbalimbali ikiwemo za pembejeo na kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.
Amesema Rais na wasaidizi wake wamedhamiria kuwaondolea kero zote zinakwamisha maendeleo ya wananchi kwa kuendeleza kazi na miradi mbalimbali inayoendelea hapa nchini.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka wakazi wa Mkoa huo kuwa tayari kushiriki zoezi la Sensa hapo mwakani katika tarehe itakayopangwa.
Amesema zoezi hilo ni muhimu kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhuu Hassan kwa ajili ya kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.