Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifungua mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo Sept 27,2021.
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo Sept 27,2021.
****************************
NA EMMANUEL MBATILO, DODOMA
Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya madiwani na watendaji wengine kwenye Halmashauri zetu,ambapo serikali imeridhia madiwani kulipwa posho kila mwezi na hii itasaidia madiwani kuacha kuhangaika fedha zinazokusanywa na kujilipa posho.
Ameyasema hayo leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu katika mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo Sept 27,2021.
Akizungumza katika Mkutano huo Rais Mhe.Samia amesema Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI imekuwa ikiongoza kwa kutengewa fedha nyingi ambapo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha TAMISEMI imetengewa kiasi cha shilingi Trilioni 7.3 takribani asilimia 20 ya bajeti yote ya serikali.
Aidha Rais Samia ameiagiza ALAT kutumia mitandao katika kazi zao kutoa taarifa za Serikali za mitaa kukusanya mapato na kuweka rekodi za huduma zinazotolewa kwa wananchi.
“Kubwa ninalogomba kwenu ni thamani ya pesa kwenye miradi, juzi Waziri Mkuu alipelekwa kwenye kibanda kilichojengwa kwa milioni kadhaa ukikitizama na fedha zilizotajwa ni tofauti, kimepakwa rangi lakini ni kibanda ambacho kingejengwa kwa Milioni 3″. Amesema Rais Samia
Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema mwaka 2021 Wanafunzi wanaomaliza darasa la saba ni takribani Milioni 1 na wanaomaliza kidato cha nne ni laki 4 hivyo kuna ongezeko la wanafunzi laki 5, ameshaelekeza Wakurugenzi wote wanafunzi wote watakaofaulu darasa la saba waanze kidato cha kwanza siku moja na hakuna Second selection.
“Tunakupongeza kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye Elimu bila malipo tumepokea Bil 62 kwa ajili ya Elimu bila Malipo na fedha zimeshakwenda katika Halmashauri zetu na ule uzushi uliosambaa kuwa hakuna elimu bila malipo tunawahakikishia wananchi kuwa Fedha zimeshapelekwa”. Amesema Waziri Ummy.