Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Malongo, akisisitiza jambo kwa wahandisi (hawap pichani), katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Prof. Ninatubu Lema, akizungumza na wahandisi (hawapo pichani), katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.
Wahandisi 632 wakila kiapo cha utii katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma
………………………………………….
Na Siti Said
WAKATI Serikali ikiendelea kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi, jitihada hizo sasa zinaelekea kufanikiwa baada ya baadhi ya wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu vinavyofundisha taaluma ya uhandisi nchini kuibuka wanafunzi bora.
Kati ya wanafunzi wahitimu 35 wa kozi za uhandisi kutoka katika vyuo Tisa vinavyofundisha taaluma hiyo, walioibuka washindi na kutukiwa tuzo katika maadhimisho ya siku ya wahandisi mwaka huu watano walikuwa wasichana.
Akizungumza katika maadhimisho ya 18 ya siku ya wahandisi yaliyofanyika tarehe 2 hadi 4 mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Prof. Ninatubu Lema, anasema kadri idadi ya wahandisi inavyoongezeka nchini, pia idadi ya wahandisi wanawake nayo inaongezeka.
“Ushahidi unaonesha kuwa kati ya wahitimu waliopewa zawadi kwa kufanya vizuri katika masomo yao mwaka huu 30 walikuwa ni wanaume na watano ni wanawake, na hii inafanya ERB kuwa imetoa tuzo kwa wahandisi bora wa kike 112 tangu mwaka 2005 kati ya 385 waliopata tuzo hizo”, amesema Profesa Lema.
Amepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali ya Norway kupitia ubalozi wake hapa nchini kwa kuhamasisha wahandis wanawake kufanya bidii katika masomo kutokana na fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wahandisi hao ambapo hadi sasa wahandisi wakike 102 wamenufaika.
Tuzo za kuwapongeza wahandisi wanafunzi zilianza mwaka 2003, lengo kuu likiwa ni kuwahamasisha wanafunzi kupenda fani za uhandisi.
Tuzo kwa wahitimu bora wa uhandisi kwa mwaka 2020/2021 kutoka vyuo vya elimu ya juu hutumia vigezo vya mhitimu lazima awe amewashinda wenzake katika fani yake, awe amepata wastani sawa au zaidi ya asilimia 80 au GPA ya 4 au zaidi.
Ambapo mwaka huu vyuo Tisa vya uhandisi vimetoa wanafunzi bora ambavyo ni Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo cha Ufundi Arusha (ACT), Ndaki ya Sayansi ya Kilimo na Teknolojia ya Uvuvi (CoAF), Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT), Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT).
Mgeni rasmi wakati wa hafla ya ugawaji tuzo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho , pamoja na mambo mengine kwenye hotuba yake alisema sera na muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha wahandisi hususani vijana wanakuwa na uwezo wa kutosha kusimamia miradi ya ujenzi inayoendelea nchini na ile inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Amezitaka taasisi zote zinazohusika na kazi za kihandisi nchini kuweka kipengele cha kuwajengea uwezo wahandisi vijana katika mikataba yote ya ujenzi itakayoingiwa na Serikali kuanzia sasa.
“Hakikisheni miradi mikubwa kama ya SGR, Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, miradi ya maji, bomba la mafuta, madaraja makubwa, ujenzi wa meli na barabara unahusisha moja kwa moja wahandisi vijana”, amesisitiza Dkt.Chamuriho.
Anabainisha kuwa Serikali imejipanga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi yake ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa sekta binafsi na Serikali kushirikiana kuwawezesha wahandisi kupata uzoefu utakaowasaidia kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
Aidha, Mgeni rasmi huyo, aliwashukuru Benki ya Dunia (WB) na Serikali ya Norway kwa kufadhili programu mbalimbali za kuwajengea uwezo wahandisi hususani wanawake na kutoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, ameitaka ERB kufanya tathimini ya maazimio yaliyofikiwa mwaka jana kuona kama yametekelezwa na hivyo kujipima katika yale matarajio yaliyofikiwa.
Pia, amezungumzia umuhimu wa kufuatilia wahandisi wahitimu wanaofanya vizuri katika masomo yao ili kuona kama wanafanya vizuri katika utendaji wa kazi zao kama ambavyo maadili ya taaluma yao yanavyowataka.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga, aliwataka wahandisi ambao bado hawajajisajili kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kufanya hivyo ili kutimiza takwa la kisheria la kutambulika.
Anasema ni vyema wahandisi kujisajili kwa sababu ni takwa la kisheria hivyo wachangamkie kujiunga na mpango wa mafunzo kwa wahitimu unaosimamiwa na ERB waweze kusajiliwa ndani ya muda mfupi wa miaka mitatu.
Kadhalika, anawasihi waajiri wa kihandisi au kampuni za kihandisi kuona namna ya kuwachukua wahitimu wa uhandisi ili waweze kupata fursa ya uzoefu jambo ambalo litawasaidia kusajiliwa na kuajiriwa.
Naye Msajili wa ERB, Patrick Barozi anasema mpaka sasa ERB imesajili wahandisi 31,729 na kati ya hao wanawake ni 3,344 sawa ana asilimia 12.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Wahandisi, Profesa Bakari Mwinyiwiwa, anasema mkutano wa mwaka huu umehudhuriwa na waandisi zaidi ya 3,000.