Baadhi ya Wafanyabiashara wa ndizi wanaosafrisha mizigo yao kutoka Mkoani Kagera kwenda Mwanza kwa kutumia meli ya New Victoria “Hapa Kazi tu” wakiwa wameshusha mizigo yao muda mfupi baada ya meli hiyo kutia nanga Bandari ya Mwanza Kaskazini.
………………………………………………………………………
Uongozi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) umewatoa hofu abiria na wafanyabiashara mbalimbali wanaosadfirisha mizigo yao kwa njia ya maji kuhusu kusimama kwa muda kwa safari za meli ya New Victoria na New Butiama zinazotoa huduma katika Ziwa Victoria.
Akitaja sababu za kusitisha safari hizo Kaimu Afisa Mtendaji wa MSCL Mhandisi Abel Gwanafyo alisema kuwa meli ya New Victoria itasitisha safari zake kwa muda wa wiki mbili huku meli ya New Butiama itasitisha safari zake kwa muda wa siku nane ambapo zitapandishwa katika chelezo ili kufanyiwa uchunguzi baada ya kutoa huduma kwa muda wa mwaka mmoja.
“Tunazipandisha kwasababu za kitaalamu, meli inapofanya kazi ndani ya maji ina muda wake wa kufanya kazi ikiwa chini ya mamlaka inayodhibiti vyombo vya majini, sasa meli hizo mbili zimemaliza muda wake wa mwaka mmoja tangu zianze kufanya kazi na zinapofanya kazi kinatolewa cheti cha ubora ambacho hudumu kwa mwaka mmoja, kwahiyo unalazimika upande kwenye chelezo ili kuchunguza kuona kama ubora bado upo kama ulivyokuwa awali, kwahiyo chombo hicho kinapanda kikaguliwe ili kithibitishwe tena na mamlaka husika yaani TASAC kama kina ubora ule ule ili kiendelee tena kufanya kazi,”
Aidha, alifafanua kuwa meli hizo zilifanyiwa ukarabati mkubwa ulioghrimu Shilingi bilioni 27.6, ukarabati uliotekelezwa na Mkandarasi KTMI Co. Ltd ya Korea Kusini na hivyo kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha matazamio (Defect liability period) na kuongeza kiuwa mapungufu madogo madogo yaliyojitokeza katika kipindi hicho ni muhimu kurekebishwa baada ya kupanda kwenye chelezo.
“La tatu ni kiufundi, kwamba ‘tear and wear’ (kuchakaa) kwa vyombo vyetu hivi vinavyosafiri majini, mwili wa meli unaozama majini huwezi ukauona kwa macho, lazima upande kwenye chelezo, natoa mfano mzuri kwamba wewe unaendesha gari lako kwamba tairi likichomoka si unakwenda gereji sasa gereji ya meli ni chelezo kwamba eneo la chini huwezi kuliona kwa macho kwamba unaweza kutumia njia nyingine kama wazamiaji lakini hawawezi kuchunguza kwa uhuru zaidi kuliko meli ikipanda kwenye chelezo.”
Mhandisi Gwanafyo alisema kuwa hayo yote yanafanyika ili kutimiza msemo wa wahenga kuwa kinga ni bora kuliko kuponya, na hivyo kila baada ya mwaka lazima vyombo hivyo vichunguzwe ili kuvijua hali yake na mapungufu yakionekana yarekebishwe kwaajili ya usalama wa abiria, mizigo na chombo chenyewe.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa MSCL Anselm Namala alielezea mpango wa kampuni katika kuboresha huduma zinazopatikana ndani ya meli ikiwemo sehemu ya burudani ya mziki wa bendi kwa kuongeza mwanamuziki mwingine wa kike tofauti na sasa kuwepo na wa kiume pekee, huduma ya chakula pamoja na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na abiria kwa kampuni.
“Usafiri tunataka iwe ni sehemu ya starehe, mtu asisafiri kwa kusikitika na kupata changamoto, kwahiyo tunatumia pia hii nafasi ya ‘docking’ (meli kupandishwa kwenye chelezo) kutatua changamoto ambazo wateja wametuletea na kuzifanyia kazi ili watakapoanza tena kusafiri wasipate shida yoyote, tunataka mtu akisafiri nasi asitusahau.” Alisema
Meli hizo zimesafirisha abiria 269,573 na tani 17,812 za mizigo tangu kuanza safari zake tarehe 16.8.2020 hadi 30.6.2021 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021. Meli ya New Victoria “Hapa Kazi tu” ikiwa imesafirisha abiria 168,797 na tani za mizigo 16,647 huku Meli ya New Butiama “Hapa Kazi tu” ikiwa imesafirisha abiria 100,776 na tani 1165 za mizigo.
Meli ya New Victoria “Hapa Kazi tu” itasitisha safari zake za kutoka Mwanza kwenda Bukoba na Bukoba Kwenda Mwanza kwa muda wa Siku 14 kuanzia tarehe 26.9.2021 hadi tarehe 9.10.2021. Wakati Meli ya New Butiama “Hapa Kazi tu” itasitisha safari zake za kutoka Mwanza kwenda Nansio na Nansio kwenda Mwanza kwa muda wa siku 8 kuanzia tarehe 11.10.2021 hadi tarehe 18.10.2021.