Joseph Lyimo
JANGA la Uviko-19 limekuja na changamoto ya kusalimiana kwa kuachiana nafasi na kutokaa karibu kwa jamii mbalimbali hasa zilizopo pembezoni, inaonekana kuwa wanafanyiwa unyanyapaa.
Tangu ugonjwa huo ulipoanza kuingia nchini Machi mwaka 2020, maisha kwa ujumla yamebadilika na kusababisha wengine waonekane kuwa wananyanyapaliwa.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Mashaka Jororo anasema watu wengi wanachukua tahadhari ya Uviko-19 ila bado kuna changamoto ya watu kuona kuwa wananyanyapaliwa.
“Ukienda kule kijiji kwetu wapo baadhi ya watu wakimuona mtu akivaa barakoa anaonekana yeye ndiye ana Uviko-10 hivyo wanamuogopa na kumnyanyapaa,” anasema Jororo.
Mkazi wa kata ya Katesh John Elias anasema hivi sasa hata kwenye gari ukiwa umevaa barakoa baadhi ya watu wanadhani kuwa unaringa au unawanyanyapaa wengine kwa kuwaona kuwa wao wana Uviko-19 hivyo unaogopa kuambukizwa.
“Mtu mwingine anakupa maandiko kuwa ukilinda nafsi yako itaangamia hivyo acha Mungu akulinde, jambo ambalo ni tofauti kwani unapaswa kujilinda kwanza mwenyewe kasha unajikabidhi kwa Mungu akulinde,” amesema.
“Hata kwenye kula mtu anaogopa kumkaribisha mtu kula naye chakula tofauti na hapo awali hii yote ni unyanyapaa uliosababishwa na Uviko-19,” amesema.
Paroko msaidizi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu, Padri Elia Kimaro aliwataka waumini wa eneo hilo kuendelea kusali kanisani hapo huku wakichukua tahadhari ya Uviko-19.
Padri Kimaro amesema janga hilo limesababisha waumini kupungua kushiriki kusali kanisani na kuwataka kuendelea kumuomba Mungu na kumtukuza bila hofu.
“Tunaendelea kuchukua tahadhari zilizotolewa na wataalamu wa afya ila tusione kanisani pekee ndiyo tunaweza kupata Uviko-19 na sehemu nyingine hakuna, siyo vyema watu washiriki ibada kanisani,” amesema.
Imamu msaidizi wa taasisi ya Masjid Noor mji mdogo wa Mirerani, Mohamed Shauri alisema viongozi wa dini wameweka wazi msimamo wao juu ya kujikinga na janga la Uviko-19.
Ustaadhi Shauri alisema jambo la mtu kulinda afya yake ni suala la wajibu na ni la lazima kwa sababu afya haina mbadala katika maisha na huwezi kufanya jambo la maana kama hauna afya.
Amesema hata katika maandiko matakatifu ya Mungu ipo aya iliyoweka wazi kabisa mambo ambayo Waislamu hawana hiari nayo ikiwemo suala zima la afya.
“Suala la ulazima wa kulinda afya zetu unapaswa kutiliwa mkazo kwenye wakati huu ambapo hivi sasa dunia nzima inapambana na janga la Uviko-19,” amesema ustaadhi Shauri.
Kiongozi wa kimila wa jamii ya wafugaji wa laigwanani Yohana Ole Tiamongoi amesema janga la Uviko-19 limekuja na changamoto mbalimbali kwenye jamii hiyo hasa suala la kusalimiana.
Ole Tiamongoi amesema kanuni za afya kuhusu janga hilo zilizotolewa na wataalamu wa afya zinakataza kugusana na kutokaribiana hivyo kuwa tofauti na mila na desturi za jamii yao.
“Sisi wafugaji tunasalimiana kwa kushikana mikono na mdogo kushikwa kichwani na mkubwa, jamii ya wafugaji kutimiza hilo inakuwa vigumu kwelikweli mtu asipofanya hivyo ataonekana wa tofauti,” amesema.