Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Kikandarasi ya Inter- Consult Ltd, inayojenga barabara ya mzunguko (Km 112.3), jijini Dodoma, akielezea jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati Waziri huyo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa wakandarasi wa Kampuni ya Kikandarasi ya Inter- Consult Ltd inayojenga barabara ya mzunguko (Km 112.3), jijini Dodoma, wakati Waziri huyo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Muonekano wa Maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko, jijini Dodoma.
………………………………………..
Serikali imesema mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko jijini Dodoma, kipande cha kutoka Nala-Veyula-Mtumba -Ihumwa (Km 52.3) na kipande cha kutoka Ihumwa-Matumbulu-Nala (Km 60), unatarajiwa kuanza wiki ijayo.
Akizungumza jijini Dodoma, mara baada ya kukagua vipande vyote viwili vyenye jumla ya Kilometa 112.3 Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa hakuna haja kuchelewa kwenye utekelezaji wa mradi huu kwani Wakandarasi wapo tayari wameshafanya maandalizi ya awali kuanza kazi rasmi na asilimia kubwa ya wananchi tayari wameshalipwa fidia na kwa wale ambao bado mchakato unaendelea.
“Mradi huu saa utaanza rasmi wiki ijayo mwezi huu wa Septemba, tumeona vifaa vingi vimeshaletwa, na wananchi wengi wameshalipwa fidia na hao wengine waliobakia mchakato unaendelea,”amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof.Mbarawa amewasisitiza wakandarasi wa vipande vyote viwili kuanza kazi haraka na kujenga kwa viwango vinavyostaili ndani ya miezi 33 badala ya 36 kama ilivyo kwenye mkataba ili kuruhusu wananchi kuweza kunufaika mapema na mradi huo.
“Wakandarasi jipangeni vizuri ili kazi hii ifanyike ndani ya miezi 33 na kwa viwango vinavyostaili, sio barabara zinajengwa baada ya mwaka au miaka miwili zinaharibika,” amesema Prof Mbarawa.
Waziri Mbarawa ametoa wito kwa wananchi watakaopata ajira kwenye mradi huo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kujituma na uaminifu ili kujenga imani kwa wakandarasi hao na hatimaye kuweza kutoa ajira nyingi kwa wazawa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Salikiheri Munisi, amesema tayari wameshaleta vifaa kwenye eneo la mradi na kufafanua kuwa kinachosubiriwa sasa ni kukamilisha baadhi ya mambo machache ili kuanza ujenzi rasmi.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda, amesema kuwa mradi wa Barabara za mzunguko Dodoma umepita kata zisizopungua 10, na baadhi ya Wananchi wameshalipwa fidia, na ameongeza kuwa hata hivyo mchakato unaendelea kuwalipa waliobakia.
Amefafanua kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi Bilioni 12.76 zimelipwa kwa jumla ya wananchi 2338 kati ya 2800, na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwalipa wale waliobakia.