Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse (wa pili kushoto) akizungumza na wachimbaji wadogo wenye ulemavu wa kusikia kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi (kulia) walipotembelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini Professa Idriss Kikula (wa kwanza kushoto) kwenye maonesho ya Teknilojia ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea kwenye uwanja Mjini Geita.
Mkalimani wa timu ya wachimbaji wadogo wenye ulemavu wa kusikia kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi akizungumza kwa ishara akitoa tafasiri ya mambo yaliyozungumzwa na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse (hayumo pichani) kwenye maonesho hayo.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini Professa Idriss Kikula (wa kwanza kulia) akitia saini kwenye kitabu cha wageni mara baada ya kumaliza ziara yake kwenye Banda la STAMICO.
Picha ya pamoja na viziwi
Picha ya pamoja na watumishi wote kutoka Katika Taasisi zilizopo chini ya STAMICO
Na: Mwandishi wetu, GEITA.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu wenye ulemavu wa kusikia kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi wameliomba Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwasaidia vifaa vya uchimbaji vitakavyowasaidia kuweza kuanza zoezi la uchimbaji katika eneo lao la nyakafuru lililopo Wilaya ya Bukombe Mkoano Geita.
Walemavu hao wametoa ombi hilo kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt Venance Mwasse wa Shirika hilo alipotembelea Banda la STAMICO akiambatana na mgeni wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini Professa Idriss Kikula kwenye maonesho ya Teknolojia ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea kwenye uwanja wa Bombambili Mjini Geita.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Lucas Moni ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Geita tayari imeshawapatia eneo la kufanya shughuli zao za uchimbaji nakwamba kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mwisho ya kusafisha eneo hilo na kujenga kambi.
“Tunamshukuru sana STAMICO kwa kuweza kutusaidia kuanzia mwanzo hadi sasa tulipofikia kwa kutupa elimu ya utambuzi wa miamba ya dhahabu, usalama na Masoko hilo tunamshukuru sana” amesema Lucas Moni.
Ameziomba Taasisi nyingine za sekta ya Madini ziige mfano wa STAMICO kuwasadia watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na masuala ya uchimbaji ili waweze kufikia malengo yao
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amewapongeza walemavu hao kwa jinsi walivyoweza kushirikiana na STAMICO nakusema kuwa
“Mpaka sasa tayari wamesha orodhesha mahitaji yao yote ikiwemo vifaa vya uchimbaji lengo likiwa kuwasaidia mpaka hatua ya mwisho”Amesema Dkt. Mwasse.
Maonesho hayo ya Teknolojia ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini ni maonesho ya Nne yakiwa na lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kujifunza Teknolojia za kisasa katika sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha na kuwainua wachimbaji wadogo.