Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Chama cha ACT wazalendo wilaya ya Shinyanga mjini kimekata rufaa kwa tume ya Taifa ya uchaguzi NEC kupinga hatua ya mgombea wao wa nafasi ya udiwani kata ya Ndembezi kuenguliwa katika mchakato huo
Akitoa taarifa hiyo katibu mwenezi wa chama hicho OMARY GINDU amesema hatua hiyo inatokana na kutoridhishwa na maamuzi ya tume ya uchaguzi ngazi ya kata kumwengua mgombea wa chama hicho bwana MVANO IDD
“Leo tumetimiza hatua nyingine ya ukataji wa rufaa kwa maamuzi yaliyotoka ngazi ya msimamizi mdogo wa uchaguzi kata ya Ndembezi tumekata rufaa jimbo kwa maana imeelekea ngazi ya Taifa na rufaa tumeifikisha leo katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi jimbo majira ya saa nne na dakika 35 Asubuhi imepokelewa, imesainiwa na tunasubiria majibu”
Akizungumzia suala hiyo mgombea wa nafasi ya udiwani katika Uchaguzi mdogo katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kupitia Chama cha ACT Wazalendo amesema pingamizi alilowekewa na CCM kwa kushirikiana na Msimamizi msaidizi ngazi ya kata, ni mpango ulioandaliwa kukihujumu Chama chake.
“Tarehe 17 mwezi wa 9 nilijaza fomu namba 10 na ndiyofomu iliyoambatanisha kwenye pingamizi na mgombea mwenzangu wa chama cha CCM iliyobandikwa katika bodi ya kunitangaza kwamba mimi ni mgombea na nimepitishwa kisheria na kwamba nilikuwa tayari nimekidhi vigezo lakini fomu namba mbili iliyobandikwa katika perfect ya picha yangu siyo ile niliyoijaza kwa mkono wangu sasa sikujua walifanya hivyo kwa makusudi pamoja na hivyo nimepitia katika misukosuko mikubwa nimetishwa nililazimishwa kujitoa lakini kwa ujasiri nilionao sikuogopa vitisho”
Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Bwana SAID BWANGA amesema chama hicho na mgombea wake hakihusiki na tuhuma zinazotolewa na Chama cha ACT Wazalendo,na kwamba tume ya Uchaguzi NEC ndiyo yenye mamlaka yote.
“Hilo mimi nakataa na nakanusha kwamba siyo kweli ni siasa za maji taka chama cha mapinduzi ni chama chenye nidhamuna maadili mema na kinaheshimu watu wote bila kubagua rangi, kabila, hisia wala itikadi za vyama vyovyote hatuwezi kuteka mtanzania kwa ajili ya kugombea au alikuwa na uwezo gani hana nguvu yoyote ya kuweza kushindana na chama. Tumeshindana na vyama 17 zote kama tungekuwa na nia ya kuteka si tungeteka mbona waliingia ulingoni na tukawachapa yeye akubali ameshindwa”
Kwa upande wake msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Ndembezi TIMOTHY ANDREW TIMOTHY amesema uteuzi wa mgombea huyo umetenguliwa kwa sababu hakukidhi matakwa ya kanuni kwa mujibu wa sharia za tume ya uchaguzi NEC ikiwemo kutoa tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi
“Sababu ambazo zimefanya huyo ndugu yetu wa chama cha ACT wazalendo awekewe pingamizi na uteuzi wake kutenguliwa ni kwamba hajatoa tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi kwa mujibu wa mashariti yaliyowekwa na sheria”
Hatua hiyo inafuatia aliyekuwa Diwani wa kata ya Ndembezi ambaye pia alikuwa ni meya katika Manispaa ya Shinyanga DAVID NKULILA kufariki Dunia mwezi uliopita