Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya ameitaka jamii kuacha tabia ya kumaliza kesi za ukatili kienyeji ambapo amesema mila na desturi kandamizi zinachangia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Mmuya amesema mashirika , wadau na taasisi zisizo za Kiserikali zishirikiane na Serikali katika kuondoa mila na desturi Kandamizi ambazo zinachangia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii
Ameyasema hayo leo kwenye ziara yake mkoani Shinyanga wakati alipo itembelea shule ya Agape inayomilikiwa na shirika la Agape Mkoa wa Shinyanga linalotetea haki za wanawake na watoto
Mmuya katika ziara yake amekutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wanawake na Watoto Mkoa wa Shinyanga pamoja na wadau wanaotekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA)
Amesema mila na desturi kandamizi zinachangia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambapo ameiomba jamii kuacha tabia ya kumaliza kesi za ukatili kienyeji huku akivishauri vyombo vya dola ikiwemo Polisi na Mahakama kukaa na kujadili namna ya kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa kesi za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
“Mila na desturi kandamizi katika maeneo mengi ndiyo inachangia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mila hizi tunaziendekeza sisi kwa kufanya vikao ngazi ya familia na kumaliza kesi za ukatili kienyeji. Tunalipana fedha na mali na kumaliza kesi za matukio badala ya kupeleka kesi kwenye vyombo vya sheria huku vyombo vya sheria navyo vikilaumiwa kuchelewesha maamuzi matokeo yake ushahidi unapotea na matukio yanaendelea kutokea kwani hakuna hatua kali zinazochukuliwa kwa wahusika”,amesema Mmuya
“Rai yangu kwa wadau,nyinyi mmebeba rasilimali fedha, rasilimali watu na ujuzi na mnaisaidia sana serikali. Kinachotufurahisha zaidi nyinyi mnakutana na wananchi moja kwa moja. Naomba mshirikiane, mtambuane, mjadili kwa pamoja masuala yanayohusu wananchi kisha mgawane maeneo ya kazi badala ya wadau wengi kujikita katika eneo moja”, amesema Mmuya.
“Tunataka Rasilimali chache zitumike kwa matokeo makubwa katika kuhakikisha tunatokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo kuondoa sifa mbaya ya kuwa na mimba na ndoa za utotoni”,ameongeza Mmuya.
Katika hatua nyingine ameupongeza Mkoa wa Shinyanga kwa kutengeneza Mpango Mkakati wa Mkoa katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wadau mbalimbali kuendendelea kushirikiana na serikali
“Shinyanga mnaendelea kufanya vizuri katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia lakini bado mna fursa ya kufanya vizuri zaidi. Niwapongeze wadau mmekuwa na ushirikiano mzuri na serikali”,amesema.