Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndg. Daniel Chongolo amewataka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuchangamka kununua mahindi kwa wakati ili kuwafanya wakulima kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Katibu Mkuu ameyasema hayo Ruvuma wilayani Mbinga wakati akiongea na wananchi na wanachama wa Chama hicho wakati wa ziara ya wajumbe wa Sekretariet ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa.
Ambapo amesema, tayari Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya Ununuzi wa mahindi hayo kwa wakulima kwa awamu ya pili.
Katibu Mkuu amesema, Rais Samia ametoa fedha za kununulia mahindi ni lazima watu wa NFRA waweze kuchangamka kwani kazi ya fedha sio kukaa katika mifuko au akaunti za Taasisi, kazi yake ni kuelekea kwenye maeneo yaliyokusudiwa.
“Mwananchi amelima shamba lake kwa bidii, kavuna vizuri mazao yake anataka kutengeneza mambo yake na anataka kujipanga na pembejeo za msimu ujao wakicheleweshwa kwenye mambo ya Msingi watakuwa hawatendewi haki.” Katibu Mkuu
“Sisi tufanye kazi yetu ya singi tununue mahindi kwa wakati,mahindi yakishanunuliwa Mwananchi atajipangia mwenyewe manunuzi yake kwa sababu fedha ni ya kwake mwenyewe,” Katibu Mkuu amesisitiza
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amewaomba wananchi wa Mbinga kulima mazao mengine ambayo yanastahimili kwenye eneo la mkoa huo ili kuendeleza kupanua wigo wa mzunguko wa kipato.