Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru akiwa katika eneo la Mto Katuma.
Sehemu ya mto Katuma iliyowekwa vizibo vya kienyeji kuzuia maji
…………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Katavi
Bodi ya maji ya bonde la ziwa Rukwa limewataka wakazi wa vijiji unapopita mto Katuma unaoipitisha maji yake katika hifadhi ya taifa ya Katavi na kupeleka ziwa Rukwa; kuacha kufanya vitendo vya uharibifu katika mto huo kwani hali hiyo inahatarisha maisha ya wanyama pori wanaoutegememea mto huo wakiwemo viboko na mamba
Kaimu Afisa Mazingira Bodi ya maji bonde la ziwa Rukwa Mathew Edson ametoa wito huo mara baada ya kukuta vizibo zaidi ya kumi katika kijiji cha Mnyagala vilivyowekwa na wananchi kwa lengo la kuchepusha maji ili kuvua samaki
Amesema jambo hilo limekuwa ni kero kwa kila mwaka ambapo wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuondoa vizibo hivyo na kuurudisha mto katika hali yake ya kawaida
‘Wakiziba maji hivi na kuyaelekeza upande mwingine mtitiriko wa maji unapungua na wanavua kambale kwa urahisi, lakini wanapoacha muda mrefu mto unakauka na maji yanashindwa kwenda ziwa Rukwa’alisema Mathew
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru amezungumza na wakazi wa kijiji cha Mnyagala na kutoa onyo kwa watu waliotajwa kuhusika na uharibifu huo
Pia aliwataka kwenda kuondoa vizbo vyote walivyoweka na kuongeza kuwa watakaporudia tena watachukuliwa hatua za kisheria
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamewalaumu kamati ya usimamizi wa bonde dogo la mto katuma kwa kudai kuwa hawako makini katika kusimamia ulinzi wa mazingira
Hata hivyo wajumbe wa kamati hiyo wameeleza kuwa wakati mwingine wanafukuzwa na mapanga wanapokuwa doria na hivyo kuhitaji waongezewe nguvu ikiwemo kupatiwa askari wa jeshi la akiba