……………………………………………
NaMathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof.
Adolf Mkenda leo tarehe 18 Septemba 2021 ametembelea na kufanya mazungumzo na Ndg
Odhiambo Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania yenye maskani yake
Kurasini Jijini Dar es salaam.
Pamoja na kujionea shehena
kubwa ya mbolea Waziri Mkenda ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji mkubwa
iliyofanya nchini na kuwarahisishia upatikanaji wa mbolea wakulima kote nchini.
Waziri Mkenda amesema kuwa
pamoja na kuongezeka kwa bei ya mbolea katika soko la Dunia lakini ameiomba
kampuni hiyo kupunguza bei ya mbolea huku akiahidi changamoto zinazoihusu
kampuni hiyo serikali yeye atazivalia njuga.
Amesema kuwa kampuni hiyo
imeendelea kujipatia faida kubwa ya uuzaji wa mbolea tangu ilipoanza kufanya
biashara zake nchini, hivyo wakati huu ambao kumekuwa na changamoto ya gharama
kubwa kwa wakulima wanapaswa kuona uwezekano wa kupunguza bei.
Prof Mkenda amezishukuru
kampuni za mbolea YARA pamoja na OCP kwa kufanya biashara kwa ufasaha mkubwa wa
mbolea ambazo zimekuwa zikifika kwa wakati na kuuzwa kwa wakulima.
“Kuna watu bado hawafahamu
wakiona bei ya mbolea imepanda wanadhani Wizara ya Kilimo au serikali
imepandisha bei jambo ambalo sio kweli kwani bei ya mbolea imepanda katika soko
la Dunia” Amekaririwa Waziri Mkenda
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Mbolea ya YARA Ndg Winstone Odhiambo ameomba kupewa muda wa siku chache ili
afanye mazungumzo na viongozi wakuu wa kampuni hiyo ili kuona uwezekano wa
kupunguza gharama kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Odhiambo amesema kuwa
serikali imefanya kazi kubwa ya kuimarisha usafiri wa reli kwani kwa
kusafirisha mbolea kwenda mikoani kwa kutumia treni kumepunguza gharama za
usafirishaji.