Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti
WAHITIMU wa Mafunzo ya Kijeshi kwa mujibu wa Sheria Operesheni Samia Suluhu Kambi ya 830 Kibiti Mkoa wa Pwani, wameaswa kulipatia heshima jina la kiongozi huyo aliyekubali kutumika jina lake kwenye mafunzo hayo.
Aidha wametakiwa wajiepushe na matukio yasiyokuwa ya kimaadili, badala yake wakawe mfano mzuri kwa wa-Tanzania, pia watangaze mazuri yanayopatikana ndani ya jeshi hilo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ,Kanali Ahmed Abbas kwenye sherehe za kuwaaga wahitimu 985 wa mafunzi ya kijeshi yaliyofanyika kwenye kikosi hicho, ambapo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) aliwakilishwa na Brigedia Absolomon Shausi yakihudhuliwa na maafisa mbalimbali wa jeshi hilo.
“Niwaombe , mafunzo mliyoyapata katu yasitumike vinginevyo, yapo mambo makuu mliyoyazungumza hapa yanayomhusu kijana, lakini la zaidi ni jina lililotumika la Operesheni Samia Suluhu Hassani ni kubwa, mkaliheshimisha jina hilo kuwa mfano bora kwa jamii,” alisema Kanali Ahmed.
Nae Brigedia Absolomon aliyemwakilisha Mkuu wa JKT Brigedia Rajabu Mabele, amewapongeza wakufunzi kwa kazi wanayoifanya kwa wahitimu hao.
“Brigedia Jenerali Mabele anawasalimia, anawapongeza kwa kuhitimu mafunzo yenu, wenyewe mmekili kwamba baadhi yenu mlikuwa watukutu, lakini leo mmeeleza kuwa mpo vizuri katika nyanja mbalimbali,” alisema Brigedia Absalomon.
Mkuu wa Kikosi hicho Meja Victor Woindumi akisoma taarifa ya kikosi hicho, imeelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miezi mitatu, ambapo wakufunzi wamefanyakazi kubwa ya kuwanoa vijana hao.
“Sina mashaka na mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi wetu, tumeshuhudia vijana wakionesha ujuzi wao walioupata ndani ya kikosi chetu cha 830 hapa Kibiti, ndugu mgeni rasmi nakuhakikishia kwamba mafunzo waliyoyapata wahitimu hawa sina mashaka nayo kwani vijana wameiva ipasavyo,” ilieleza taarifa ya Meja Woindumi.
Awali taarifa ya wahitimu hao iliyosomwa na Monica Alphonce akisaidiana na Hassan Selemani imeeleza kuwa wamepata mafunzo mbalimbali, yakiwemo ya jeshi kwa nadhalia na vitendo, ambayo yamewawezesha kumaliza wakiwa timamu.
“Katika kipindi chetu tulichokuwa katika mafunzo tumeshiriki mafunzo na kazi mbalimbali ikiwemo kujenga majengo hapa kikosini, likiwemo jengo la Utawala pamoja na kushiriki kikamilifu katika kilimo,” ilimalizia taarifa ya wahitimu hao.