Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano huo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge akizungumza katika mkutano huo.
…………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
SERIKALI imesema kuwa mpango wa elimu bila malipo ,hautasitishwa kama baadhi ya watu wanavyozusha ambapo maneno hayo ni ya uzushi.
Hayo yalisemwa wilayani Mkuranga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi kwenye shule ya Sekondari Mwandege.
Mwalimu alisema kuwa mpango wa elimu bila malipo utaendelea na hautasitishwa na wananchi wasisikilize maneno ya uzushi kwani serikali ya awamu ya sita ya Samia Suluhu itaendelea na mpango huo.
“Mfano ni wilaya ya Mkuranga kupitia bajeti ya wizara ya elimu imeipatia kiasi cha shilingi milioni 326 kwa ajili ya shule za msingi na milioni 200 kwa shule za sekondari kwa ajili ya mpango huo,” alisema Mwalimu.
Alisema kuwa hadi Julai mwaka huu kiasi cha shilingi milioni 114 tayari zimeshatolewa kwa ajili ya mpango huo wa elimu bila ya malipo kwa wilaya hiyo.
“Wanasema elimu bure chini ya Samia itakufa wanaosema hivyo washindwe na walegee kwani jambo kama hilo halipo ambapo serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya mpango huu,”alisema Mwalimu.
Aidha alisema serikali itatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mbili ambapo fedha zinazotolewa ni shilingi milioni 600 kwa kila jimbo nchini.
“Tumeona shule hii ina wanafunzi wengi na tumeona shule hii iko jirani na Dar es Salaam na wengi wanatoka huko serikali itatoa fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari hivyo mtapate shule mbili,” alisema Mwalimu.
Katika hatua nyingine ameunga mkono ujenzi wa stendi ya kisasa kwa ajili ya mabasi yanayokwenda mikoa ya Kusini kwani mabasi hayo kwa stendi ya Mbagala inakuwa imezidiwa.
Alisema kuwa hata barabara ya mwendokasi iishie hapo ili kuipunguzia stendi ya Mbagala wingi wa magari ambapo mabasi hayo hayana stendi maalumu na hapa stendi iitwe Samia Suluhu Hassan.
Awali mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kuwa wamedhamiria kuongeza wigo wa kukusanya mapato kwani ndiyo yanayofanya mambo ya maendeleo yafanyike.
Kunenge alisema kuwa wamedhamiria kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kutatua changamoto kwenye mkoa ili ibaki historia.
Naye mkuu wa wilaya ya Mkuranga Hadija Ally alisema kuwa wilaya imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 11,700 Mbezi kwa ajili ya uwekezaji.
Ally alisema kuwa wanatarajia kuboresha wa hospitali ya wilaya kuwa kituo cha afya ili kukabiliana na wingi wa wagonjwa pamoja na kuomba kujengwa kituo cha afya Mwandege.