MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilida Buriani ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Sikonge kuwaondoa watoto wote ambao wanaishi katika eneo la uchimbaji madini la Kitunda na kuwapeleka Kijijini kwa ajili ya usalama wao.
Alisema lengo ni kuwaondoa katika hatari mbalimbali zinazoweza kuwakabili kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini na kuhakikisha wanakwenda kuishi Kijijini ambapo watapata huduma za elimu.
Balozi Dkt. Batilida ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea eneo hilo kwa ajili ya kujionea Kibanda ambacho kianzishwa na wachimbaji wa madini na baadhi ya watendaji wamekuwa wakishinikiza kuanzishwa kwa shule ya Msingi.
“Watoto wote na mama zao waliomo kwenye Mgodi wanatakiwa kuondoka na kwenda Kijijini …humu mgodini watabaki wanaume…ni makosa watoto kuendelea kuishi humo…tukiwakuta tena tutalizimika kusitisha shughuli za uchimbaji ,jambo ambalo hatuki litoke” alisisitiza.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilida aliagizwa kubomolewa kwa Kibanda kilichojengwa katika eneo la Mgodi kwa kutaka kukigeuza Shule ya Msingi.
Alisema Kibanda hicho kilipojengwa ni hatari kwa watoto kwa kuwa kipo karibu eneo la kuchanganyia kemikali kwa ajili ya kuchenjulia dhahabu na pembeni yake kuna shimo lenye maji yenye kemikali hatari zinatumika kusafishia dhahabu ambazo ni hatari kwa maisha ya bianadamu.
Balozi Dkt. Batilida aliongeza karibu na Kibanda hicho upo mchanga ambao una mabaki ya kemikali ambazo zimetumika kuchenjuliwa dhahabu na hivyo kuhatarisha maisha ya watoto kama wakiushika.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inatoa shilingi milioni 900 kila mwezi kwa ajili ya bure kwa Mkoa wa Tabora.
Balozi Dkt. Batilida alisema kufuatia hali hakuna haja ya kuwa na kibanda hicho kwa kuwa Shule ambayo ni rasmi ya Misheni ipo katika Kijiji cha Kitunda nayo inapata fedha kwa ajili ya elimu bure.
Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Batilida ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma wa Mistu Tanzania(TFS) kukagua maeneo yote ili kujiridhisha kuwa hakuna wananchi wanaishi ndani yake na kuendesha shughuli kinyume cha Sheria za Uhifadhi na nyingine za Nchi.
Alisema sanjari hilo ameiagiza Ofisi ya Madini kupitia migodi yote ya Mkoa wa Tabora ili kuhakikisha hakuna vitendo ambavyo vinavunja Sheria za Nchi vinafanyika katika maeneo hayo ikiwemo vya ujenzi wa vibanda kwa ajili ya shule zisizo rasmi.
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu alisema Watumishi ambao walishindwa kusimamia taratibu na kuachangia wananchi wajenge Kibanda hicho kinyume cha Sheria mbalimbali katika eneo hilo watachukuliwa hatua.
Alisema taratibu za uanzishaji Shule zinajulikana na zipaswa kufutwa pindi wananchi wanataka kuanzisha Shule katika eneo lao.
Makungu alisema Mtendaji wa Kata na Afisa Elimu Kata wameshindwa kusimamia majukumu yao na ndio maana watoto wamejaa katika eneo la Mgodi wakati walipaswa kuwa katika Shule rasmi.