Na Asila Twaha -DODOMA
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dkt. Festo Dugange amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanafuata sheria, taratibu na miongozo katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na Matumizi ya fedha wanazo kusanya katika Hospitali Pamoja na Vituo vya afya nchini, huku akionya matumizi ya pesa kabla ya kupelekwa Benki.
Dkt. Dugange amesema hayo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesema, ukusanyaji wa mapato mazuri huisaidia serikali kuendelea kupanga mipango ya kutatua changamoto ya kujenga miundombinu ya Afya, pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
“Bado siridhishwi na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa Sekta Afya hasa wale waliopewa mamlaka ya kusimamia kuanzia ngazi ya Mkoa na Halmashauri kwa kuendelea kutokufuata sheria, taratibu na miongozo waliyopatiwa, kwani baadhi yenu mmekuwa mkienda kinyume na malengo ya serikali hasa kwakushindwa kusimamia kikamilifu mapato yatokanayo na uchangiaji wa fedha za Afya kwenye maeneo yenu, amesema Dkt. Dugange.
Naibu Waziri Dugange amesema kumekuwepo na hoja nyingi sana za kutopeleka fedha benki, na badala yake kunatumika zikiwa mbichi bila kufuata taratibu za fedha za Serikali, hivyo “naelekeza kila mmoja wetu kwa nafasi yake akahakikishe anaweka mpango mkakati wa kudhibiti upotevu wa mapato kuanzia kwenye ukusanyaji hadi kwenye matumizi” alisisitiza Dkt. Dugange
Dugange ameendelea kusema, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuhakikisha miundombinu bora ya Sekta Afya inaimarishwa na wananchi wanapata huduma hasa kwa upande wa dawa kwa serikali kuendelea kutoa fedha na kuhakikisha dawa zinapatikana katika vituo vya Afya.
Sambamba na hilo Dkt. Dugange amewataka viongozi hao wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kujikinga na kuipokea chanjo ya ugonjwa wa UVIKO -19.
Mkutano Mkuu wa waganga wakuu wa Mikoa, uliodumu kwa muda wa siku tatu, ulikuwa na kaulimbiu isemayo “Ustahamilivu wa Mifumo ya Afya katika Mapambano dhidi ua UVIKO-19 ‘Changamoto na Fursa’’.