*****************************
Na Mwamvua Mwinyi,KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani ,Sara Msafiri ameeleza kuandika wosia siyo uchuro kwani unasaidia kuondoa migogoro na kuepusha watoto kukosa haki zao za msingi mara baada ya kiongozi wa familia kufariki dunia.
Aidha amesema baadhi ya akinamama wamekosa haki zao kwa kutokujua taratibu za kisheria mara inapotokea migogoro ya ndoa.
Msafiri aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa vijiji, mitaa na kata juu ya mauala yakiwemo usajili wa ndoa, talaka, usimamizi wa mirathi, uandishi na utunzaji wa wosia na muunganisho wa wadhamini na taratibu zake yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Alisema kuwa baadhi ya ndoa zimekuwa na changamoto na kusababisha baadhi ya wanandoa kuuana hivyo wanapaswa kumtanguliza Mungu na kufuata taratibu za kisheria ili watambulike kisheria kuliko kuishi kienyeji.
Hata hivyo ,alibainisha kuwa moja ya changamoto ya ndoa ambayo aliishuhudia ni mume ni kuua mke wake kisha kumchoma kwa mkaa ambapo aliweka magunia manne ya mkaa kisa walikuwa na ugomvi kwa miaka mine ambapo kila mtu alikuwa anakaa chumba chake.
“Kisa cha kumuua eti alikuwa akifikiria ametumia fedha nyingi kupata mali halafu mke akidai talaka inabidi wagawane ndiyo sababu kuu ya kumuua na kujifanya mke wake kapotea hivyo kuna haja ya viongozi kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mazima ya ndoa ”alisema Msafiri.
Akizungumzia juu ya wosia alisema kuwa siyo uchuro bali ni kuweka mazingira mazuri hata kiongozi wa familia akifa warithi wake kila mtu atajua haki yake iko wapi na nini atarithi kutokana na jasho lake na wasitoe wosia wakiwa kwenye hali mbaya au wengine wakiwa hoi hospitalini ambapo pia baadhi ya wasimamizi wa mirathi wengine wanawatapeli warithi halali.
“Tumeshuhudia baadhi ya watu ndani yafamilia wakiibuka bada ya kiongozi wa familia kufa akidai za marehemu naye anasehemu ya kurithi na kuwaacha watoto au mke ambao ndiyo warithi halali wakihangaika kama vile marehemu hakuacha chochote,”alisema Msafiri.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Haki za Kisheria wa (RITA) Lina Msanga alisema kuwa baaadhi ya watu wamekuwa wakihofia kutoa wosia wakidai kuwa ni uchuro ambapo ni mwarobaini wa wale wanaoudhulumu mali za marehemu ambapo kuna wosia 810 umehifadhiwa kwao.
Msanga alisema kuwa ili kuhakikisha familia zinaishi kwenye hali nzuri wanatoa elimu kwa viongozi mbalimbali hapa nchini ili wasaidie kuelimisha jamii juu ya masuala ya familia na haki za jamii ambapo kuna mashauri 104 kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi.