Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisaini katika Kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Muleba, Mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikagua mradi wa kikundi cha wanawake Upendo cha Kata ya Magata, Wilaya ya Muleba kinachojishughulisha na mradi wa kuongeza thamani mazao ya samaki kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato binafsi na familia.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila akipokea zawadi ya Samaki aina ya Sangara kutoka kwa mmoja wa wanakikundi cha wanawake wajasriamali wa Kata ya Magata, Wilayani humo ikiwa ni sehemu ya utambuzi wa mchango wake katika maendeleo ya biashara yao kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akishuka bonde mara baada ya kukitembelea kikundi cha Wanawake Upendo, Kata ya Magata, Wilayani Muleba, Kagera kulia Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila na kushoto ni Katibu wake, Rehema Kassimoto.
Picha zote na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, WAMJW
**************************************
Na Mwandishi Wetu, Muleba
Wazee wa Kijiji Ikondo, Wilayani Muleba Mkoa wa Kagera wameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na baadhi ya Watoto kuwatelekeza Wazazi wao mara baada ya kuzeeka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, Wazee hao wamesema uzee unaambatana na changamoto mbalimbali za maisha hivyo, Serikali iwanusuru na maisha ya utegemezi kwa kuweka mazingira rafiki kwao ili wazeeke kwa staha.
Pia wameiomba Serikali kupitia vifungu vya Sheria ili viweze kuwapa nafuu kwa kuwalazimisha watoto na jamaa zao kutoa matunzo kwa wazazi wao baada ya kuzeeka kama vile Sheria inayowabana wazazi wanapowatelekeza na kuacha kuwatuza watoto.
Akijibu hoja za wazee hao, Naibu Waziri, Mwanaidi amesema Serikali inatambua na kuenzi Wazee kwa kuwa wao ni tunu kwa Taifa na uitaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuwatunza kwa kuwapatia huduma stahiki hasa huduma za afya ili waishi maisha mazuri na yenye faraja.
Amesema kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 ili kumaliza malalamiko na dukuduku za wazee kuhusu mstakabali wa maisha yao.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea vikundi vya kiuchumi na uzalishaji mali vya Wanawake wadogo mjini Muleba na Kikundi cha Wanawake Upendo kinachojishughulisha na kuongeza thamani ya samaki katika Kata ya Magata.
Awali akizungumzia hali ya Wazee Wilayani Muleba, Mkuu wa Wilaya hiyo, Toba Nguvila amesema Wazee wana mahitaji mengi ikiwa ni pamoja na huduma za tiba, kushiriki katika mijadala ya Mabaraza yao hivyo Wilaya inahakikisha wazee wanaangaliwa kwa namna ya kipekee ili wasikose huduma hizo muhimu.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, juzi nimezungumza na Wazee wangu hawa, wamenipa maombi mengi kama ulivyoyasikia na kwa vile umefika naomba baadhi niyatue kwako na kwa kuwa mko katika hatua za maamuzi huko mbele kutakuwa na majibu kwa wazee wetu” alisema.