Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalua katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
………………………………………
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imekiri uwepo wa ongezeko la biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ushoroba wa kusini zikiwemo nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalua amesema kuwa ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Kenya, Burundi na Uganda umeongezeka na kwamba ushirikiano kati ya Tanzania na Mataifa hayo umezidi kuimarika ukiashiria kukua kwa diplomasia ya uchumi.
“Sasa hivi ukiangali ukuaji wa biashara chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, Serikali inaishirikisha ipasavyo Sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini,” amesema Bi. Ngalua
Ameongeza kuwa ushirikiano ambao Serikali imekuwa ikiutoa kwa sekta binafsi umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na ushoroba wa kusini ikihusisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Bi Ngalua amepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuamua kuambatana na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika Taasisi ya Sekta Binafsi kwa kuwa hatua hiyo imesaidia kuwakutanisha na kuwaunganisha na wenzao wa Mataifa mengine tofauti na nyakati zilizopita ambapo kila mfanyabiashara alijitafutia fursa peke yake.
Kwa uapnde wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameihakikishia Taasisi ya Sekta Binafsi ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini kwa kuwa Serikali inaamini uwepo wa sekta binafsi imara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi imara wa Nchi.
Balozi Mulamula ameitaka TPSF kuhakikisha kuwa inakuwa na kanzi data ili kurahisisha azma ya Serikali ya kuiunganisha sekta hiyo na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka katika mataifa mengine ulimwenguni.
Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan Oswald aliyefuatana na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo ya Uchumi.
Dkt. Oswald amemuambia Balozi Mulamula kuwa Tanzania imekuwa ni Nchi ya kwanza kwa viongozi hao wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani kuifanya na hiyo imetokana na ishara ya mabadiliko ya kidiplomasia na ushirikiano wa Maendeleo na Mataifa mengine duniani iliyooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa mazungumzo kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan na Kansela wa Ujerumani Mhe Angela Merkel ambayo yalilenga kutoa kipaumbele cha uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yamekuwa kichocheo cha Viongozi hao kufanya ziara hapa nchini.
Dkt.Stefan amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania pamoja na Nchi za Afrika kuzisaidia kuimarisha uchumi kutokana na kuathiriwa na UVIKO 19.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yaligusia masuala la ulinzi na usalama katika ukanda wa maziwa makuu na kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wa Burundi