Waziri mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za hisani zilizoandaliwa na Benki ya NMB.
Mbio hizo maarufu kama NMB marathon zinalenga kukusanya kiasi cha Tsh/= Bilioni 1 ndani ya miaka minne, zitakazosaidia matibabu ya Fistula kwa wanawake wasio na uwezo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba tisa, afisa mkuu wa wateja binafsi na biashara za kati Filbert Mponzi, amesema NMB kwa kushirikiana na hospitali ya CCBRT pamoja na wadau wengine, watafanikisha mbio hizo ambapo mgeni rasmi atakuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.
“Tunashukuru waziri mkuu Kassim Majaliwa amekubali kushiriki katika marathon hii kwahiyo yeye atakuwa mgeni wetu rasmi, ambapo mbio hizi zitaanzia leaders club” amesema Mponzi.
Mponzi ameongeza kuwa wananchi wote ambao wapo tayari kushiriki mashindano hayo wanapaswa kujiandikisha ili nao wawe sehemu ya kuwachangia wanawake wenye fistula. “Uwandikishaji kwa wale wote wanaotaka kushiriki mbio hizi kuwasaidia wanawake wenye changangamoto ya fistula waendelee kujiandikisha kwani watakuwa wameshiriki kuwapa tabasamu”. Ameongeza mponzi.
Hadi sasa zaidi ya Tsh. Milioni 226 zimekusanywa ambapo lengo ni kukusanya Bilioni moja kwa miaka minne ili kuhakikisha wanawake wenye fistula wanapata matibabu stahiki. Mbio hizo za hisani zenye kauli mbiu ya ‘mwendo wa upendo’ambazo zilitarajiwa kufanyika Septemba 18, zitafanyika Septemba 25 mwaka huu ili kuongeza muda wa wananchi kujiandikisha kwaajili ya kushiriki.