Edda Sanga aliyekuwa mwelimishaji na mtoa mada katika smeina ya waandishi wa habari na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) akiwasilisha mada katika semina hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Sheraton zamani New Africa mwishoni mwa siki hii.
Josephine Arnold Mwanachama wa TAWLA na Mratibu wa Miradi akitoa maelezo ya awali kuhusu Semina hiyo ya waandishi wa habari na Chama cha Wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA)
Mwandishi Elikunda Materu akiwasilisha majumuisho ya kundi lao na matarajio baada ya semina hiyo.
Picha zikionesha baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika semina hiyo.
CHAMA Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA,) kimewakutanisha wanahabari na kujadili nafasi zao katika kuonyesha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi katika kuhakikisha kunakuwa na usawa katika ushiriki wa shughuli za kiuchumi.
Akizungumza katika warsha hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam mwanahabari mkongwe Bi. Edda Sanga alisema kuwa nafasi ya mwanamke na ushiriki wake katika shughuli za kiuchumi ni mkubwa sana na kuwataka wanahabari hao kuwafikia na kuzionesha juhudi hizo zinazofanywa na wanawake katika jamii hasa katika shughuli mbalimbali hasa za kiuchumi na siasa.
”Wanawake wanahitahi fursa, haki, usawa na ustawi na hili linajidhihirisha wazi wanawake wanajihusisha katika shughuli za uzalishaji mali kwa asilimia 90.4 kupitia kilimo hasa cha jembe la mkono, na wanakidhi mahitaji ya chakula kwa nchi nzima kwa asilimia 70 Pia tunaona wanawake wanavyopambana katika sekta nyinginezo ikiwemo mifugo, uvuvi, ushonaji, ufumaji na ususi.
Bi. Edda aliwataka wanahabari kuwaibua wanawake waliopambana na kuleta matokeo chanya katika jamii, taifa na familia zao kwa ujumla ili kuleta chachu kwa mabinti ili kujenga taifa imara lenye haki na usawa hasa wa ushiriki wa shughuli za kiuchumi na biashara.
Katika warsha hiyo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi na biashara, vikwazo na namna ya kuwafikia wanawake wengi zaidi na kuvumbua jitihada zao zinazoleta matokeo chanya katika jamii ili kuleta chachu kwa mabinti wanaochipukia.