Ofisa Usajili wa BRELA Ruth Mmbaga (wa pili kushoto) akimkabidhi Leseni ya Biashara Dkt. Hamis Mahuna (wapili kulia) mara baada ya kufika katika Banda la BRELA na kupatiwa huduma ya kusajili jina la Biashara na kupewa Cheti chake Papo kwa papo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyomalizika leo katika viwanja vya ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.(wa kwanza kulia) ni Ofisa Leseni Wa BRELA Robert Mashika, na (wa kwanza kushoto) ni Ofisa Tehama wa Wakala huyo Hillary Mwenda.
Ofisa Usajili wa BRELA Ruth Mmbaga (kushoto) akimkabidhi Leseni yake Mteja aliyefika kwenye Maonesho hayo Bw. Fulgensi L. Fulgensi mara baada ya kusajili jina la Biashara na kuweza kupatiwa Leseni yake Papo kwa papo.
Dkt. Hamis Mahuna (kulia) akizungumza na Maofisa wa BRELA Ofisa Usajili Ruth Mmbaga (wa kwanza kishoto aliyesimama), na Ofisa Tehama Hillary Mwenda (wa pili kushoto aliyekaa) alipokuwa akiwashukuru Maofisa hao mara baada ya kufanikiwa kusajili jina la Biashara na kupewa Leseni yake Papo kwa papo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyomalizika leo Jijini Dar es Salaam.
Ofisa Leseni wa BRELA Robert Mashika (kulia) na Ofisa Tehama Hillary Mwenda (kushoto) wakijadiliana jambo mara baada ya kufanikisha kumaliza zoezi la kusajili majina mbalimbali ya Biashara na kutoa Leseni katika maonesho hayo.
Ofisa Tehama wa BRELA Hillary Mwenda akiendelea na Majukumu yake. (PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo imehitimisha rasmi zoezi lake la kusajili na kutoa Leseni za Biashara Papo kwa papo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyokuwa yakifanyika kwa siku tano katika viwanja vya ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwahudumia watu zaidi ya 200.
Akizungumza leo katika maonesho hayo Ofisa Leseni wa BRELA Robert Mashika amesema kuwa watu mbalimbali wameweza kujitokeza kusajili majina ya Biashara na Makampuni na kupatiwa elimu.
“Katika siku hizi za maonesho haya tumekuwa na muda mzuri wa kutoa elimu na kujibu maswali mbalimbali ya wananchi na tumeweza kuwahudumia watu zaidi ya 200” amesema Mashika.
Mmoja wa wateja waliohudumiwa na kupatiwa Cheti chake papo kwa papo ni Dkt. Hamisi Mahuna aliyekuwa na ndoto ya kuanzisha huduma za Afya amsema kuwa ndoto zake zimetimia kwani yeye alifika ili ajue taratibu za kufuata lakini amejikuta amefanikiwa kufanya usajili na kupewa Leseni yake kwa muda mfupi.
“Mimi kwanza nawashuru sana wafanyakazi wa BRELA wamenisaidia sana na kwakweli wanafanyakazi kwa ufanisi wa hali ya Juu sana leo hii nimefika hapa wameweza kuthibitisha jina langu la Biashara na kunisajili hapa hapa hili limenifurahisha sana” amesema Dkt. Mahuna huku akionesha kufuraha yake.
Ameongeza kuwa Taasisi ya BRELA imekuwa ikifanyakazi kubwa hasa kwa kujikita kutoa Elimu kwa wananchi na hivyo kuwasihi watumishi wa Taasisi hiyo kuendelea kufanyakazi bila kuchoka kwani wananchi wanaimani kubwa na Taasisi hiyo.
Kumalizika kwa Maonesho hayo kunaipa fursa BRELA kujipanga tena kwenda kupiga kambi ya siku kumi Mjini Geita yatakapofanyika maonesho mengine makubwa ya Teknolojia ya Sekta ya Madini yanayotanariwa kuanza tarehe 16 hadi 26 Septemba mwaka huu huku timu nyingine ikipiga kambi Jijini Mwanza kwenye maonesho ya 16 ya Biashara ya Afika Mashariki yaliyoanza August 28 na kumalizika Septemba 5 mwaka huu.