******************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
Hanang’. MASHINDANO ya Mount Hanang’ Cup yanatimua vumbi Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, yakihusisha michuano ya kandanda, riadha na mpira wa pete.
Mbunge wa jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amesema mashindano hayo ya kutangaza mlima Hanang’ unaoshika nafasi ya nne kwa urefu hapa nchini yatachangia kuibua vipaji vipya vya wanamichezo mbalimbali wa soka, riadha na mpira wa pete.
Mhandisi Hhayuma amesema mashindano hayo yatahusisha wanamichezo chipukizi wa riadha, soka na pete kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vyao ili wafike mbali ikiwemo ngazi ya kimataifa.
Amesema kuanzishwa kwa michezo hiyo mbalimbali kutasaidia kuinua vipaji na kuweza kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa kama Olimpiki na kuhamasisha wananchi kutembelea mlima Hanang’.
“Tumeita michuano hii Mount Hanang’ Cup kwa ajili ya kuutanga mlima wetu na pia tunataria tutapiga hatua kimichezo na wanamichezo kupata fursa ya mashindano haya,” amesema mhandisi Hhayuma.
Amesema michezo hiyo itakuwa inafanyika kila mwaka hivyo wachezaji chipukizi watapita hatua kubwa japokuwa michezo ina changamoto mbalimbali ila kupitia wadau watafanikisha kufika mbali.
Amewahimiza wananchi wa eneo hilo kushiriki michuano hiyo kwa kufika kwa wingi ili kupata burudani na kupata taarifa mbalimbali za mlima Hanang’.
Mmoja wa wafanyakazi kwenye hifadhi ya mlima Hanang’ John Masatu amesema watatumia michezo hiyo kukuza utalii wa ndani kwa wananchi wa Hanang’ mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla ili kuongeza kipato cha nchi.
“Mlima Hanang’ una msitu mzuri mno, maporomoko ya maji na vivutio mbalimbali vinavyowafaa watu kupumzika hivyo kupitia mashindano haya vijana watakuza vipaji na kutangaza mlima wetu,” amesema Masatu.
Amesema wanamichezo mbalimbali wa hapa nchini, wakiwemo wa timu za Simba, Yanga na Azam, wanapaswa kufika Hanang’ kwa ajili ya kutembelea na kufanya mazoezi kwani hali ya hewa ya eneo hilo inaruhusu.
Mchezaji wa timu ya soka ya Endasak, Mathew Bayo amempongeza mhandisi Hhayuma kwa kuandaa michuano hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine itakuza vipaji vya eneo hilo.