Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kulia) na Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali (wa pili kushoto) wakisaini moja kati ya hati 6 zinazohusu makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi katika masuala ya fedha. Anayeshuhudia katikati ni Makamu wa Rais wa (SMT) Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Mwanasheria Mkuu (SMT) Prof. Adelardius Kilangi na wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mjini Unguja.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kulia) na Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali (wa pili kushoto) wakionesha moja kati ya kati ya hati 6 zinazohusu makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi katika masuala ya fedha. Anayeshuhudia katikati ni Makamu wa Rais wa (SMT) Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Mwanasheria Mkuu (SMT) Prof. Adelardius Kilangi na wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mjini Unguja. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Zanzibar)
…………………………………….
Na Rahma Taratibu, WFM, Zanzibar
SERIKALI ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeweka historia baada ya kusaini mikataba tisa ikiwa ni sehemu ya hoja 11 za muungano zilizopatiwa ufumbuzi.
Hafla ya utiaji wa saini wa mikataba hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi kilichopo Unguja-Zanzibar na kushuhudiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo tisa kunafanya hoja za Muungano zilizotatuliwa mpaka sasa tangu mwaka 2006 kufikia 18 kati ya hoja 25 zilizokuwepo hatua iliyoelezwa kuwa itadumisha zaidi Muungano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Miongoni mwa mikataba iliyosainiwa inahusu mikataba sita
inayogusa masuala ya fedha na uchumi ikiwemo mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje, mikataba ya mkopo wa mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na Mkataba wa mkopo wa Ujenzi wa Barabara ya kutoka Chakechake hadi Wete Pemba.
Miradi mingine ni mkopo kwa ajili ya ujenzi Bandari ya Mpigaduri, mkataba wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za Simu unaofanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar pamoja na mapato yanayokusanywa na Idara ya Uhamiaji-Zanzibar ambayo yatatumika Zanzibar badala ya kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Aidha, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ameshuhudia utiwaji saini wa mikataba mingine mitatu ambayo ni Mkataba wa Uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu, Mkataba wa Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano na Mkataba wa uingizaji wa maziwa ya Azam kutoka Zanzibar kwenye soko la Tanzania Bara.
Hoja nyingine za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi lakini hakukuwa na mikataba ya kusainiwa ni pamoja na uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Kodi na Uteuzi wa Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana kutoka Zanzibar.
Dkt. Mpango ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuharakisha utatuzi wa hoja za Muungano zilizosalia zinazohusu masuala ya fedha kama vile kodi za vyombo vya moto na masuala mengine.
Mheshimiwa Mpango alitaja faida za kutatuliwa kwa changamoto hizo za masuala ya Muungano kuwa ni pamoja na kuimarisha muungano huo wa kihistoria, kukuza shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili za Muungano, na kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar kwa kuboresha shughuli zake za kiuchumi na kuvutia uwekezaji na kuboresha mazingira mazuri ya biashara.
Aliipongeza kamati iliyohususisha mawaziri na makatibu wakuu kwa pande zote mbili za Muungano kwa kazi nzuri ya kutatua hoja hizo za Muungano.
Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria na kuongeza kuwa kutatuliwa kwa kero hizo za Muungano kutazidisha imani kwa wananchi wa pande zote mbili.
Pia aliwatoa wasiwasi wananchi wanaolalamika kwa maamuzi ya masuala ya maamuzi yalikuwa yanatolewa upande mmoja na kwamba kufanyika kwa vikao hivyo kunadhihirisha kuwa maamuzi ya masuala ya muungano yanafyika kwa kuzisjirikisha pande zote mbili za Muungano.