Na Marco Maduhu, Shinyanga
Askofu wa Makanisa ya International Evengelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) David Mabushi, amewataka vijana wa Kanisa hilo kumtumikia Mungu kipindi cha ujana wao, ili wapate baraka katika maisha yao.
Askofu Mabushi amebainisha hayo leo Jumapili Agosti 22,2021 kwenye hitimisho la wiki ya vijana kanisa la IEAGT ambao wameendesha ibada yote.
Amesema kipindi cha kumtumikia Mungu ni cha ujana na hivyo kuwataka vijana wa Kanisa hilo, wamtumikie Mwenyezi Mungu pamoja na kutangaza kazi yake na kuokoa watu ili waijue kweli.
“Ukitaka kuwa na maisha ya ushindi, lazima ujipange katika siku zako za ujana ndipo kwenye maono, ukishakuwa mzee utabaki kuwa na simulizi tu,” amesema mchungaji Mabushi.
Naye, Mwenyekiti wa Idara ya Vijana wa Kanisa la IEAGT Peres Mbogoma, amesema kwa juma zima wamefanya vitu mbalimbali, ikiwamo kutembelea kiwanda cha Jambo pamoja na kutoa msaada wa chakula kwa watoto wenye uhitaji, ambao wanalelewa katika kituo cha Buhangija Mjini Shinyanga.
Aidha, akitoa Mahubiri Janet Yohana, amewataka waumini wa Kanisa hilo, wajitoe kwa bwana, na kutoa muda wao na mali, pamoja na kumtolea Zaka na Sadaka zilizo nona, ili wabarikiwe katika maisha yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti Msaidizi waIdara hiyo ya vijana Kanisani hapo Alfred Benjamini, akisoma taarifa amesema wapo 83, na wamekuwa wakifanya vitu mbalimbali, ikiwamo kuinuana karama na kufanya kazi ya Mungu.