Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Meneja wa Kampuni ya Jumbo Lindi, iliyopewa lesene ya kuchimba madini kinywe ‘Graphite’ Paul Shauri, bade ya kutembelea eneo hilo lililopo katika kijiji cha Matambarare Ruangwa, Mkoani Lindi, Agosti 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wachimbaji wadogo, eneo la Mgodi wa Dhahabu Namungo, Ruangwa, Mkoani Lindi, Agosti 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia eneo la Mgodi ambalo litachimbwa madini kinywe ‘Graphite’ lililopo katika kijiji cha Matambarare Ruangwa, Mkoani Lindi, Agosti 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya, akimfafanulia jambo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye eneo la Mgodi ambalo litachimbwa madini ya kinywe ‘Graphite’ lililopo katika kijiji cha Matambarare Ruangwa, Mkoani Lindi, Agosti 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mgodi wa dhahabu wa Namungo kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri yatakayowawezesha wachimbaji wadogo kunufaika.
Pia, Waziri Mkuu ameagiza mmiliki wa mgodi huo, afike Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma Septemba 10, 2021 akaeleze mipango yake ya kuendeleza mgodi huo pamoja na wachimbaji wadogo.
Ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Agosti 20, 2021) alipotembelea mgodi huo uliopo wilayani Ruangwa, Lindi akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo.
Waziri Mkuu amesema uongozi wa mgodi huo umeingia mikataba na wachimbaji wadogo hivyo amewataka waweke mazingira mazuri yatakayowawezesha wachimbaji hao kunufaika.
“Lazima kuwe na mikataba ambayo pia inawapa fursa wachimbaji wagodo kuchimba na kujipatia kipato na haya ndiyo malengo ya nchi. Rasilimali hizi ni za Watanzania wote.”
Amesema Serikali inawajibu wa kusimamia mikataba kati ya wachimbaji wadogo na mwenye mgodi na iwapo mikataba hiyo haitekelezwi vizuri italazimika kuangalia upya leseni hiyo.
“Fanyeni shughuli zenu kwa kuzingatia mikataba halali inayozingatia sheria za nchi. Jipangeni vizuri kwa sababu Serikali itaendelea kusimamia haki zenu ikiwa ni pamoja na mikataba.”
Waziri Mkuu amesema eneo hilo ni muhimu kwa sababu mbali na Serikali kunufaika kwa kukusanya mapato pia wananchi wengi wameweza kupata ajira katika mgodi huo.
Akizungumza na wananchi katika eneo linalotarajiwa kujengwa mgodi wa graphite katika kijiji cha Matambarare, Waziri Mkuu amewataka wachangamkie fursa ya uwepo wa mgodi huo.
Naye, Naibu Waziri wa Nishati Profesa Shukuru Manya amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali ya madini iliyoko nchini.
Amesema mkoa wa Lindi ikiwemo wilaya ya Ruangwa kuna utajiri mkubwa wa madini ya aina mbalimbali. “Namungo kuna leseni nne za uchimbaji wa kati lakini imetoa nafasi kwa wachimbaji wadogo 500.”
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni Lindi Jumbo inayochimba madini ya graphite Paul Shauri amesema mgodi huo utaanza kuzalisha ifikapo Agosti, 2022.
Amesema sehemu ya fedha za ujenzi wa mradi huo wamekopa kutoka benki ya CRDB na kwamba wamepanga kuanza kulipa deni hilo la shilingi bilioni 46 baada ya kuuza madini hayo.
Meneja huyo ameongeza kuwa “sasa ni muda wa kuanza kufikiri utaratibu wa kutafuta wazalishaji wa betri za simu ambazo zinatokana na madini haya”
Naye, Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya Kusini Denis Moleka amesema wametoa mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa ni mkombozi kwa Watanzania.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea shule Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia, na kuelezea namna Serikali iliyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuendeleza sekta ya elimu hasa kwa watoto wa kike.
“Rais ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike na kumlinda katika kipindi chake chote kuanzia chekechekea, na ndoto zake ziende hadi zitimie, Tunahitaji kupata viongozi wanawake kwenye taifa hili, pia tunahitaji wataalam wa sekta mbalimbali” Alihitimisha Majaliwa.