………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ameagiza uchunguzi ufanyike wa zaidi ya shilingi milioni 30 fedha za uuzaji wa viwanja 400 na mashamba 204 ya Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro.
Makongoro amesema mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera afanye uchunguzi wa ubadhirifu huo unaodaiwa kufanyika kupitia uongozi wa kijiji hicho wa mwaka 2018/2019.
Amesema ili viongozi wa sasa wa kijiji hicho wasionekane wamefuja fedha hizo na serikali ibaini vyema mapato hayo, hakuna budi uchunguzi ufanyike.
“Mimi kwenye fedha za umma nakuwa mkali kweli kweli, namuagiza mkuu wa wilaya afuatilie hili ili tubaini mapato na matumizi ya fedha hizo yapoje,” amesema Makongoro.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro, Ally Mohamed Kidunda amesema wananchi wa Terrat wanalalamikia matumizi ya fedha za uuzaji wa mashamba na viwanja vyao.
Kidunda amesema katika viwanja 400 kila kiwanja kiliuzwa shilingi 150,000 na kupatikana shilingi milioni 6 na mashamba 204 kila moja iliuzwa shilingi 100,000 na kupatikana shilingi milioni 20.4.
“Wananchi wanahoji juu ya matumizi ya fedha hizo shilingi milioni 30 ambazo nyingine zimetumika kwenye ujenzi wa jengo la baba, mama na mtoto la zahanati ya kijiji cha Terrat bila kubainishwa vyema,” amesema Kidunda.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera, ameahidi kufutilia suala hilo kwa kuchunguza kisha kufanikisha majawabu ya fedha hizo.
“Tuna ahidi kutuma vyombo vyetu kuchunguza hilo japokuwa nimeshapata taarifa ya benki juu ya akaunti ya kijiji ili kufahamu namna fedha zilivyoingia na kutoka kwa kipindi hicho,” amesema Dkt Serera.
Mganga mfawidhi wa zahanati ya kijiji cha Terrat, Dkt Ndiday Laizer amesema jengo la baba, mama na mtoto limefikia hatua ya lenta na kugharimu shilingi milioni 41.3.
Laizer amesema wananchi wa kijiji cha Terrat walichangia shilingi milioni 35, mfuko wa jimbo shilingi milioni 3, mkuu wa wilaya shilingi milioni 1.2 na mkuu wa mkoa shilingi milioni 2.