Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, akizungumza na waandishi wa habari
………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
AGIZO la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Julai 7 Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, la shughuli zote za uuzaji na uongezaji thamani wa madini kufanyika Mirerani linaendelea kutekelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, ameyasema hayo wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya muelekeo wa uanzishwaji wa soko la madini ya Tanzanite Mirerani Wilayani Simanjiro.
Makongoro amesema agizo la Waziri Mkuu Majaliwa la shughuli zote za ununuzi na uongezaji thamani wa madini ya Tanzanite, kufanyika Mirerani baada ya siku 90 linaendelea kutekelezwa ambapo wafanyabiashara 49 wamefungua ofisi Mirerani.
“Majengo mawili yameshatengwa kwa ajili ya uuzaji wa madini hayo na yameshaanza kutumiwa na wafanyabiashara 49 wa madini hayo,” amesema Makongoro.
Amesema hatua zinazoendelea ni upimaji wa eneo la kanda maalum ya kiuchumi (Manyara Special Economic Zone) ili kuwagawia wafanyabiashara wa madini waweke miundombinu yao na maeneo ya makazi.
Amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuingiza miundombinu muhimu ya kuwezesha huduma za maji, umeme, barabara na nyingine kama itakavyohitajika.
Amesema pia kupitia eneo hilo lililotengwa limepangwa kuwa na huduma muhimu za kijamii zikiwemo hoteli, migahawa, kituo cha polisi na maegesho ya magari.
“Nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan la kuhamishia soko la madini eneo la Mirerani Wilayani Simanjiro,” amesema Makongoro.
Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kujiongezea vipato binafsu na wale wafanyabiashara wa madini amewakumbusha kulipa kodi na maduhuli ya serikali kwa mujibu wa sheria za kodi zilizopo.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amesema utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, vikundi, wilaya, mkoa na nchi kwa ujumla.
“Jambo hilo ni kubwa na muhimu hivyo wote tushirikiane kwa ajili ya kuhakikisha kuanzishwa Tanzanite City katika eneo la Manyara special economic zones linakamilishwa ipasavyo na kwa wakati uliopangwa,” amesema Dkt Serera.
Amesema wiki ijayo atakutana na wafanyabiashara hao 49 katika kuhakikisha shughuli zote za uuzaji madini hayo yanafanyika Mirerani kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema Serikali ya wilaya ipo tayari na wataendelea kusimamia kikamilifu ili watu waweze kuanza kunufaika moja kwa moja na amewasihi watumie fursa hiyo vizuri ili serikali waweze kwenda pamoja kwani kukamilika kwa hilo utasaidia kuimarisha uchumi.
Waziri Mkuu Majaliwa, Julai 7 mwaka huu, akiwa kwenye ziara yake mji mdogo wa Mirerani, aliagiza shughuli za uuzaji na uchakataji wa madini ya Tanzanite, ambayo duniani yanapatikana Mkoani Manyara, ufanyike mji mdogo wa Mirerani pekee.