****************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Kamati ya bunge ya bajeti imetembelea Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili ambapo wameeleza kilio chao kikubwa kuwa ni kuwepo kwa mfumo wa teknolojia ya ETS ambao umekuwa wa gharama kubwa.
Wamesema kuwa, kwa mwaka wanatumia zaidi ya bilioni 20 tofauti na awali ambapo walikuwa wakitumia shilingi bilioni 2 kwa ajili ya utambuzi na kuhesabu bidhaa wanazozizalisha.
Akiwasilisha changamoto hiyo mbele ya kamati ya Bunge Mkurugenzi wa masuala ya ushirika na maendeleo endelevu wa TBL Messiya Mwangoka amesema kuwa mfumo huo unaobandika stika na kuhesabu bidhaa wanazozalisha unamilikiwa na mtu binafsi tofauti na awali stika hizo zilikuwa zikibandikwa na TRA kwa gharama nafuu.
“Changamoto kubwa ya ETS ni gharama, inatugharimu fedha nyingi kwa bidhaa zetu kuhesabiwa tuu, tumewaonesha na tuna matumaini mtaenda kutoa ushauri kwa wizara husika ili tuweze kusaidika na hii bilioni 20 ni malipo ambayo tunamlipa mkandarasi ambaye anahusika na mfumo huu na sio serikali,” Amesema Mwangoka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Daniel Baran amesema kamati hiyo imesikia changamoto hizo ambapo wao kama wazalishaji wameona ETS na baadae watakaa waone ni kwa namna gani wanaweza kuishauri Serikali ili nayo pamoja na wenye viwanda waweze kunufaika zaidi.
“Tumetembelea TBL kujionea uzalishaji uliopo mahali hapa lakini kubwa Ni kujifunza kuhusu mfumo wa ETS ambayo unatumika katika uzalisha na mfumo huu unaisaidia serikali kwa upande wa TRA kupata kiwango sahihi cha uzalishaji katika kiwanda,”Amesema Baran.
Amefafanua kuwa, kwa bahati nzuri wenye kiwanda wamekiri wenyewe kuwa walishakaa na waziri wa fedha na mipango na kumweleza changamoto hiyo na Waziri akaunda kamati kwaajili hiyo hiyo watasubiri taarifa ya kamati ndipo waone ni namna gani wataweza kuishauri serikali.
Hata hivyo kamati hiyo ilitembelea kiwanda cha Mega Beverages kinachojishughulisha na uzalishaji wa vinywaji vikali,ambapo kimeiomba Serikali kuhakikisha kuwa upandishaji wa kodi unafuata sheria ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wa kodi ili Serikali pamoja na walipa kodi kwa pamoja waweze kunufaika.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Chris Ndosi akizungumza mbele ya kamati hiyo, amesema kuwa kodi inapopanda bila wao kushirikishwa inakuwa ngumu kwao kwani wanahofia endapo watapandisha bei ya bidhaa ghafla itapelekea kupoteza wateja hali inayoweza kuathiri ustawi wa kiwanda.
Hata vivyo kamati hiyo kupitia mwenyekiti wake Daniel Baran imeahidi kuchukua changamoto hiyo ambapo wataenda kupitia na kuiwasilisha kwa Serikali.