NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii,Mwanaidi Khamis, akizungumza na waandishi wa Habari leo August 5,2021 jijini Dodoma ambapo Maafisa ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya jamii wametaliwa kuwahamasisha wazee wote nchini kujitokeza kupata chanjo ya UVICO-19 kwa hiari yao katika vituo vinavyotoa chanjo hiyo.
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki,akijibu swali mara baada ya Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii,Mwanaidi Khamis,kutoa taarifa kwa waandishi wa Habari leo August 5,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na watoa huduma katika sekta ya Afya nchini wametakiwa kuhakikisha wazee wanapewa kipaumbele katika kupata huduma ya chanjo ya ugonjwa wa Uviko -19 bila.
Kauli hiyo imetolewa leo August 5,2021 na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza na waandishi wa Habari amesema kuwa miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele katika kutekeleza mpango huo wa kinga ni wazee.
Amesema kuwa Wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Uviko 19 hivyo wanastahili kulindwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama wa afya zao.
“Nitumie nafasi hii kuwaagiza Maafisa Ustawi na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuhakikisha wanawahamasisha wazee kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo mabaraza ya wazee yaliyoko katika maeneo yao ili wapate elimu kuhusu namna ya kupata chanjo hiyo katika vituo vilivyopangwa” amesema Mhe. Mwanaidi.
Hata hivyo ameeleza umuhimu wa kuwalinda na kuwaelekeza wazee namna ya kupata chanjo ya UVIKO 19 kutokana na umuhimu wao katika maendeleo ya taifa ndio maana Serikali kwa wamu ya kwanza ya kutoa chanjo imewapa kipaumbele.
“Kwa kuwa uzee na kuzeeka unaambatana na upungufu wa kinga ya mwili, Serikali inatoa wito kwa wazee wote nchini kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya chanjo ya UVIKO 19 inayotolewa bure katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa”amesema
Pia ameyataka Mashirika na Asasi za kiraia zinazotoa huduma kwa wazee kuandaa na kuendesha Programu mbalimbali za kuhamasisha wazee kwenda kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari yao ili kuimarisha kinga katika miili yao.
”Naitaka jamii kuwahamasisha wazee wote kwa hiari yao kwenda katika vituo vya kutolea chanjo ili wapate huduma hiyo”amesisitiza
Hata ameisisitiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia miongozo kutoka kwa wataalamu wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki amesema kuwa Serikali itahakikisha kundi la wazee linasimamiwa vizuri katika kupata huduma ya chanjo ya UVIKO 19 ili kulilinda kundi hilo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.