Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda,akifungua kikao cha wadau wa huduma za msaada wa kisheria chenye lengo la lengo la kujadiliana juu ya masuala ya huduma za msaada wa kisheria uliofanyika jijini Arusha.
Msajili wa Wasaidizi Huduma za kisheria,Felister Mushi ,akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa huduma za msaada wa kisheria chenye lengo la lengo la kujadiliana juu ya masuala ya huduma za msaada wa kisheria uliofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda,(hayupo pichani) wakati akifungua kikao cha wadau wa huduma za msaada wa kisheria chenye lengo la lengo la kujadiliana juu ya masuala ya huduma za msaada wa kisheria uliofanyika jijini Arusha.
…………………………………………………..
Na.Faustine Gimu Galafoni.
Serikali kupitia Wizara ya katiba na sheria imesema upo mpango wa kuwa na madawati ya msaada wa kisheria kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa huduma za msaada wa kisheria chenye lengo la lengo la kujadiliana juu ya masuala ya huduma za msaada wa kisheria ambapo amesema hii yote ni katika kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa wananchi katika maeneo yote na vyombo vyote vya upatikanaji haki.
“Kwa upande wa Mahakama, Wizara iliingia makubaliano na Mahakama katika kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana. Upo mpango wa kuwa na madawati ya msaada wa kisheria kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu hii yote ni katika kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa wananchi katika maeneo yote na vyombo vyote vya upatikanaji haki”amefafanua.
Katika hatua nyingine amesema Masuala ya msaada wa kisheria ni masuala mtambuka hivyo wadau wote wanalo jukumu la kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati na kwa kila mwenye uhitaji.
“Serikali inatambua mchango wenu mkubwa unaofanywa katika kuhakikisha wananchi wanafikia haki kwa wakati. Ni jukumu letu sote kuwafikia wananchi wa ngazi za chini kabisa kwa wote waliopo mijini na vijijin, hata hivyo tuangalie zaidi wale walio pembezoni kwani ndiyo walio na uhitaji mkubwa zaidi. Hawa wa mjini wanafursa ya kusikia kupitia redio mbalimbali na hata kuona vipindi mbalimbali vya elimu ya kisheria kwa umma kupitia televisheni”amesema.
Aidha,Naibu waziri huyo amesema Lugha ya Kiingereza imekuwa na kikwazo na manyanyaso kwa mwananchi wa hali ya chini kunyang’anywa haki zake hivyo Mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki vitaanza kutumia lugha ya Kiswahili katika uendeshaji wa mashauri na nyaraka mbalimbali za mahakama ikiwemo hukumu na mienendo ya Mahakama ili kuweza kumsaidia mwananchi wa hali ya chini.
Hivyo, Serikali kwa kutambua suala hili imeanza kufanyia kazi kwa kuanza kutafsiri sheria zote kutoka lugha ya kiingereza kwenda Kiswahili kwa lengo la kueleweka kwa urahisi kwa wananchi na kuwataka wadau wa sheria kutumia Kiswahili bila woga.
“Wananchi wetu wengi hawana uelewa wa masuala ya kisheria jambo ambalo linapelekea wengi wao kupoteza haki kwa kukosa mwongozo sahihi wa namna ya kupata haki zao. Serikali kwa kutambua suala hili imeanza kufanyia kazi kwa kuanza kutafsiri sheria zote kutoka lugha ya kiingereza kwenda Kiswahili kwa lengo la kueleweka kwa urahisi kwa wananchi, Si hivyo tu, Mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki vitaanza kutumia lugha ya Kiswahili katika uendeshaji wa mashauri na nyaraka mbalimbali za mahakama ikiwemo hukumu na mienendo ya Mahakama”amesema.
Ameendelea kufafanua kuwa watoa huduma ya msaada wa kisheria wapatao 182 na wasaidizi wa kisheria wapatao 657 wameshasajiliwa mpaka sasa ambapo ni katika mwaka wa nne wa utekelezaji wa Sheria ya msaada wa kisheria ambayo ni Sheria Na. 1 ya Mwaka 2017 na Kanuni zake za Mwaka 2018.
Hata hivyo,Naibu waziri huyo amewataka wasaidizi wa kisheria ambao hawajajisajili kufanya mchakato wa kujisajili ili kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kutoa huduma za msaada wa kisheria katika maeneo yaliyosahaulika hususan vijijini .
“Ninafahamu wengi wa watoa huduma mliopo hapa mmeshajisajili na kutambuliwa na Serikali. Kwa wale ambao bado, niwaombe wajisajili chini ya matakwa ya sheria ya msaada wa kisheria. Kujisajili kunaipa Serikali kuwa na takwimu sahihi juu ya watoa huduma waliopo ili kuimarisha mifumo ya kiutendaji na kufanya maamuzi ya kisera kuhusiana na masuala ya msaada wa kisheria”amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wadau wa sheria akiwemo Felister Mushi Msajili wa watoa Huduma ya msaada Kisheria pamoja na Tolbert Mmasy-Mkurugenzi mtandao wa wasaidizi wa kisheria Tanzania [TAPANET]wamesema mkutano huo ni muhimu katika kujadili masuala mbalimbali ya sheria zenye changamoto na kuweza kuzifanyia maboresho.
Miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na huduma ya Msaada wa kisheria kabla ya kutungwa Sheria ya Msaada wa kisheria Na.1 ya mwaka 2017 pamoja na maboresho ya huduma ya Msaada wa kisheria chini ya Sheria ya Msaada wa kisheria Na 1 ya mwaka 2017.