NA.ELISA SHUNDA,DODOMA.
KUACHIANA vijiti katika uongozi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake ni sehemu ya utendaji kazi na demokrasia iliotukuka na demokrasia katika kuleta mawazo mapya yatakayoweza kusaidia chama au jumuiya kusonga mbele na kutimiza lengo la ilani ya CCM ya wakati uliopo.
Kwa muktadha wa demokrasia na uongozi uliotukuka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Wazazi Tanzania ambayo ni jumuiya ya chama hicho, Ndugu. Gilbert Kalima, amekabidhiwa rasmi ofisi na vitendea kazi vyote kutoka kwa Katibu mkuu mstaafu, Erasto Sima, katika ofisi za makao makuu ya jumuiya hiyo Jijini Dodoma, leo.
Katibu mkuu mstaafu wa jumuiya ya wazazi mstaafu, Erasto Sima, akizungumza wakati akimkaribisha katibu mkuu mpya wa jumuiya hiyo, ndugu.Gilbert Kalima, alisema anashukuru kwa kupata nafasi ya kutumikia nafasi hiyo kuna mambo kadha wa kadha ya kiofisi na kijamii ambayo ameyafanya nchi nzima na amewaomba wafanyakazi wa jumuiya hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha katibu mkuu huyo mpya.
“Binafsi kwa niaba ya familia yangu ninakishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuniamini na kunikabidhi nafasi hii ya ukatibu mkuu wa jumuiya ya wazazi toka mwaka 2018 hadi mwaka huu 2021, hivyo nisipokuwa na shukrani kwa nafasi hii nitakuwa sina shukurani, nikupongeze kwa nafasi hii nakutakia kazi njema” alisema Sima.
Akizungumza baada ya kukaribishwa, katibu mkuu mpya wa jumuiya ya wazazi, Ndugu.Gilbert Kalima, alimshukuru katibu mkuu mstaafu, Sima, kwa kusema amepokea kijiti hicho cha nafasi ya ukatibu mkuu wa jumuiya ya wazazi na ameahidi kuitumikia nafasi hiyo katika kuleta maendeleo chanya kwa manufaa ya jumuiya hiyo.
“Nashukuru kwa kukaribishwa siku ya leo katika ofisi hii, ninafahamu changamoto ni nyingi katika jumuiya yetu ila kwa umoja wetu tukishirikiana tutavuka viunzi vyote vinavyotukabiri, sisi ni wazazi ndio tegemeo la busara kubwa kwa chama chetu;
“Tujifunge mkanda kwa pamoja kazi iendelee kwa kushirikiana na chama chetu pamoja jumuiya nyinginezo katika kuhakikisha tunatimiza lengo la ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan”, alisema Kalima.